Prof. Sospeter Muhongo
*Ni kwa wanavijiji wanaoishi jirani na bomba la gesi Mtwara - Dar
SERIKALI imeamua kupunguza
kwa kiasi kikubwa bei ya kuunganisha umeme majumbani na kufikia sh.
27,000/ kwa wanavijiji wanaoishi kwenye maeneo ambayo bomba la gesi
linapita.
“Jana Waziri
Mkuu aliagiza tutafute namna ya kuwasaidia wananchi wanaoishi jirani na
njia ya bomba la gesi. Nami nilikaa na wasaidizi wangu jana usiku na
kufanya hesabu na tukaamua tuweke kiwango hicho kwa ajili ya wakazi
hao,” alisema.
Alisema katika mikoa mikoa mingine gharama za
kuunganisha umeme ni sh. 177,000/- lakini kwa mikoa ya Lindi na Mtwara
gharama hizo zilishushwa na kufikia sh.99,000/-. “Lakini sasa hawa
wenzetu tumewapa upendeleo zaidi na tumewapunguzia gharama hizo hadi sh.
27,000/-,” alisema huku akishangiliwa.
Gharama hizo ni maalum kwa ajili ya wakazi waishio
jirani na bomba hilo linaloanzia Mtwara hadi Dar es Salaam kupitia mikoa
ya Lindi na Pwani.
Akizungumza na mamia ya wakazi wa Mangaka waliofika
kushuhudia uzinduzi huo, Waziri Mkuu alisema uzinduzi wa mradi huo wa
umeme ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuhakikisha kila wilaya
inapata umeme.
“Mpango wa kupeleka umeme nchi nzima ni wa miaka mitatu
na katika sekta ya Nishati chini ya Mpango wa Matokeo Makubwa ya Haraka
(BRN), tumeazimia kwenda kwa awamu ili tuwafikie wananchi wengi zaidi
kutoka asilimia 24 ya sasa hadi kufikia asilimia 30 ya watumiaji wa
umeme,” alisema Waziri Mkuu.
Akitoa taarifa
juu ya mradi huo wa umeme wilayani Nanyumbu, Meneja Mwandamizi wa
TANESCO, Kanda ya Dar es Salaam na Pwani inayojumuisha mikoa ya Lindi na
Mtwara, Eng. Mahende Mugaya alisema mradi huo umegharimu sh. bilioni
5.6/- na unatarajiwa kukamilika Aprili, mwaka huu.
Alisema
kuzinduliwa kwa mradi huo kunafanya wilaya zote za mkoa wa Mtwara ziwe
zimepata umeme wa kuanzia na kwamba kazi itaendelea kupitia Wakala wa
Umeme Vijijini (REA) ili kuongeza idadi ya watumiaji wa umeme kwenye
mkoa huo.
“Chini ya
mfuko wa REA tumetenga sh. bilioni 7.6 ili zitumike kusambaza umeme
katika wilaya zote za mkoa wa Mtwara ambao sasa hivi watumiaji wa umeme
wamefikia 15,675 sawa na asilimia nne ya wakazi wote wa mkoa huu.”
Alisema katika mwaka 2012-2013 walipata wateja 2,609
tofauti na idadi ya zamani ya wateja 1,300 ambayo ilikuwa imezoeleka.
Alisema hivi sasa wamepokea maombi kutoka kwa wateja 2,588 ambao tayari
wamekwishalipia gharama za kuunganishiwa umeme.
Chini ya mradi
wa umeme kupitia REA, jumla ya vijiji 54 katika wilaya za Tandahimba,
Masasi na Newala vitanufaika na mradi huo ulioanza kutekelezwa Desemba
2013 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 2015.
(mwisho)
0 comments:
Post a Comment