KAMPUNI ya Bia Tanzania(TBL) imezitaka
Halmashauri mbali mbali nchini ambako miradi mingi ya kijamii inatekelezwa
kutokana na misaada ya Wahisani kutoa uangalizi ili iwe endelevu kwa manufaa ya
wananchi ambao ndiyo walengwa.
Ombi hilo limetolewa na Afisa Uhusiano
wa Kampuni ya Bia ya TBL, Doris Malulu,wakati akikagua mradi wa uchimbaji wa
Kisima cha Maji uliofadhiliwa na Kampuni hiyo katika kituo cha Afya cha
Tunduma kilichopo Wilayani Momba Mkoa wa Mbeya.
Doris alisema maeneo mengi wanapeleka
miradi ambayo Serikali ilitakiwa kuifanya ambapo baada ya kufanikisha miradi
hiyo na walifadhili kuondoka miradi hiyo hufa kutokana na kukosekana kwa
uangalizi toka Serikalini.
Alisema ili miradi iwe endelevu na
imnufaishe mwananchi aliyekusudiwa ni vema suala la uangalizi likawa shirikishi
kwa kila mtu ambapo itakuwa misaada kwa vizazi vijavyo na kwamba kampuni hiyo
imelenga kituo cha Afya kwa kuwa ndiyo kimbilio la Watu wengi.
Aliongeza kuwa msaada wa kisima hicho
unagharimu zaidi ya Shilingi Milioni 24, ambapo alisema TBL imetoa msaada huo
ikiwa ni sehemu iliyojiwekea ya kurudisha fadhila kwa jamii kutokana na faida
wanayopata kutokana na mauzo ya bidhaa zao.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Mji mdogo wa Tunduma, Helen Kagamizi, aliishukuru Kampuni ya Tbl
kwa msaada wa kisima cha maji katika Kituo cha Afya kwa kile alichosema Mji wa
Tunduma unatatizo kubwa la uhaba wa maji.
Alisema mradi huo utakapoanza
kufanyakazi utakuwa mkombozi kwa watu wengi hususani wagonjwa ambao ndiyo
wahitaji sana wa Maji na kwa mujibu Mkandarasi anayechimba kisima
hicho anasema kinaweza kuzalisha Mililita 5000 kwa saa.
Naye Mganga wa Kituo hicho Dk. Gibson
Mbaza alisema Tbl imetoa msaada mkubwa na muhimu katika sekta ya afya kwa
sababu huduma hiyo inahitaji huduma ya maji kwa wingi kutokana na mahitaji ya
usafi kwa wagonjwa na mazingira kuhitaji maji mengi.
Aliongeza kuwa maji hayo watayatunza
vizuri ili yaweze kuwasaidia katika shughuli za kila siku za matibabu na
wagonjwa kutokana na kukabiliwa na upungufu wa maji safi na salama kwa mji
mzima wa Tunduma.
Na Mbeya yetu
|
0 comments:
Post a Comment