Thursday, 30 January 2014

WATANZANIA WAKABILIWA NA UPUNGUFU WA MKUBWA WA MAJI

 
MAJJJJJJJ_093d2.jpg
Sehemu za ndani ya mikoa ya Tanzania zikiwa kame.
Watanzania wanalaani hali ya hewa na kuongezeka kwa joto wakati usambazaji wa maji mijini ukidorora na huku mabishano yakizidi kuwa makali baina ya wakulima na wafugaji kuhusu matumizi ya vijito katika maeneo yao.
 
Taarifa nyingi za kitaalam siku za nyuma zilionya kuhusu uongezekaji wa mahitaji ya maji na viwango vya maji yanayopatikana lakini tahadhari hizo ama zilipuuzwa au hazikutiliwa maanani ipasavyo.
Mara nyingi wanasiasa walibeza tahadhari hizo bila kufikiri pale walipowapotosha wananchi wao kuvamia mazingira yaliyohifadhiwa ili wakate miti, kuanzisha makazi au kulima mashamba karibu na vyanzo vya mito.
Miji ambayo imepanuka kwa haraka katika maeneo ambayo hapo awali yalikuwa na vijito vingi, kama vila Morogoro na Tanga katika ukanda wa mashariki, sasa inapata adha nyingi kuanzia mazingira machafu mpaka uhaba wa shughuli za kiuchumi kutokana na ukosefu wa maji.
Jiji kuu la biashara na viwanda, Dar es Salaam, pia limekumbwa na adha hizo. Mamia ya wakazi wa jiji hili hutumia saa nyingi kila siku wakitafuta maji. Matatizo yao huenda yasikomee hapo kadiri gharama za upatikanaji maji zinavyozidi kupanda siku hadi siku.
Mameneja wa rasilimali hii pia wanasumbuka kuziba mabomba yanayovuja huku wakipambana na wizi wa maji pale ambapo watu hujifungia mabomba isivyo halali, wakati viwango vya maji vikishuka kule yanakotoka kabla ya kuingizwa katika mifumo ya usambazaji.
"Uhai wetu, ustawi wetu, afya zetu na maendeleo yetu vyote hutegemea upatikanaji maji safi na salama pale tunapoishi. Wakati umefika tuone kila anayeharibu chanzo cha maji ni adui," amesema Profesa Jumanne Maghembe, Waziri wa Maji wakati wa kuzindua mradi wa maji katika manispaa ya Moshi.
Waziri huyo aliongeza kuwaTanzania imepoteza viumbe hai na mimea kwa wingi katika kipindi cha miaka miwili iliyopita kutokana na uharibifu wa mazingira asili ambayo yalihifadhi vyanzo vya maji.
Hivi karibuni athari za kukauka kwa mito zimewasibu wananchi katika sehemu mbalimbali za Tanzania. Hata hivyo hakuna juhudi thabiti zinazofanywa na jamii au asasi za serikali kukabili athari zaidi za kimazingira, kijamii, kiuchumi na hata za kisiasa ambazo huenda zikasababishwa na hali hii.
Mto wa Ruaha ambao ulikuwa na maji mengi kila mwaka ni mfano dhahiri. Viongozi wa kitaifa ambao huambaa mto huu wakiwa katika magari wanaposafiri kwenda au kutoka mikoa ya kusini ya nchi, sana sana hushangaa wakisema kuwa mto hauungurumi tena kama zamani.
Mto huu ulikuwa maliasili kubwa ambayo iliwezesha taa kuwaka na viwanda kuzalisha mali kwa gharama ya chini katika miji mingi kutokana na umeme uliofuliwa kwa maji ya Bwawa la Mtera na kituo cha umeme cha Kidatu katika Mkoa wa Morogoro.
Bila mto huu, nini itakuwa hatima ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na shughuli za kitalii ambazo hivi karibuni zimepanuka katika eneo hilo? Hili ni baa ambalo linaanza kujitokeza lakini linazuilika ikiwa hatua makini zitachukuliwa kuwa na mifumo endelevu ya kilimo na kudhibiti matumizi ya maji ya Ruaha kwa kilimo cha umwagiliaji cha mpunga.
Watu wengi huharakisha kulaumu mabadiliko ya tabia nchi kwa kila mkasa hata kama wamekosa kuwa waangalifu wenyewe katika mwenendo wao wa maisha katika mazingiza yao.
Majadiliano kuhusu mkataba wa kimataifa juu ya mabadiliko ya hali ya hewa, ambao unategemewa kufikiwa na mataifa yote mwaka 2015, bado yanasuasua kutokana na kutoaminiana baina ya nchi zilizostawi na zile zinazoendelea.
Ili Tanzania iaminike katika jukwaa la majadiloiano hayo ya kimataifa, watumishi wake wa umma ambao hutetea maslahi ya taifa hapana budi wajumuike na viongozi wa jumuia za wananchi pamoja na wanasiasa kuonyesha kuwa wanao utashi wa kisiasa kupunguza athari za mabadiliko ya hali ya hewa katika ngazi ya taifa.
CHANZO:DWSWAHILI

0 comments: