Friday, 31 January 2014

RC IRINGA AAGIZA WANAFUNZI WALIOSHINDWA KURIPOTI SEKONDARI NA WAZAZI WAO WAKAMATWE


Mkuu wa mkoa  wa Iringa Dr Christine Ishengoma katikati akitoa maagizo ya  kukamatwa kwa  wazazi na wanafunzi  walioshindwa  kupeleka  watoto  wao  Sekondari.

MKUU  wa  mkoa  wa  Iringa Dr Christine Ishengoma  ameagiza  viongozi  wa vijiji ,kata  ,tarafa na wilaya  kuwachukulia  hatua  kali  wazazi  na  wanafunzi  walioshindwa  kujiunga na kidato cha kwanza  pamoja na kuchaguliwa .


Mkuu  huyo  wa mkoa  alitoa agizo hilo leo  wakati  akifungua  kikao cha kamati ya  ushauri ya mkoa  wa Iringa kilichofanyika katika ukumbi  wa Siasa  ni  Kilimo mjini  Iringa na kuhudhuriwa  na  waziri wa  nchi  ofisi ya  Rais ( Utawala  bora )George  Mkuchika.


Alisema kuwa  wazazi  wa  wanafunzi  waliofaulu kujiunga na elimu ya  sekondari mwaka  huu ni  vema  kuhakikisha  wanawapeleka  watoto wao  shule  vinginevyo utaendeshwa msako  mkali wa  kuwabaini  wanafunzi  ambao  wameshindwa  kuanza elimu ya  sekondari  ili  kuwachukulia hatua kwa kuwafikisha mahakamani.


Kwani  alisema kuwa  mkoa  hautapenda  kuona  wanafunzi hao  waliofaulu  kujiunga na elimu ya  sekondari  wakiendelea  kubaki  nyumbani huku  wenzao  wakiendelea na masomo ya  sekondari.


Hivyo  alisema kwa  kuwa ni wajibu wa kila mzazi  kumpatia  elimu  mtoto  wake  serikali  haitasita  kuchukua hatua kwa  mzazi atakayeshindwa  kusomesha mtoto  elimu  ya msingi na sekondari  .


Dr Ishengoma  aliwataka  wazazi  wote  wenye  watoto  wanaotakiwa  kujiunga na elimu ya msingi na wale  waliochaguliwa  kwenda  sekondari  kuhakikisha  wanatimiza  wajibu  wao kabla ya  serikali  kuchukua hatua ya  kuwafikisha  mahakamani kwa kushindwa  kusomesha   watoto . 


Hata  hivyo mkuu  huyo wa mkoa  alipongeza  jitihada  mbali mbali  zinazofanywa na Halmashauri  ya Manispaa ya  Iringa katika kuendelea  kuboresha  elimu kwa kuifanikishia  Halmashauri  hiyo kushika nafasi ya tano kitaifa .


Dr Ishengoma  alitaka  kuandaliwa kwa  zawadi  kwa ajili ya Halmashauri  hiyo pamoja na  zawadi  nyingine kwa Halmashauri ya Kilolo kwa  kushika nafasi ya mwisho  kimkoa .


katika  hatu  nyingine  mkuu  huyo wa  mkoa aliwataka  wananchi  wa Halmashauri ya Manispaa ya  Iringa  ambao wanamiliki magari  kuhakikisha  wanalipa  ushuru wa maegesho katika mji  huo na iwapo watashindwa  kulipa ushuru  huo ni vema  wakaacha magari yao nyumbani na kuja mjini kwa usafiri wa daladala ama kwa miguu.


Mkuu  huyo alisema  kuwa kumekuwepo na usumbufu mkubwa kwa  watu  waoakusanya ushuru  kusumbuliwa na baadhi ya  wamiliki wa magari  ambao  wamekuwa  wakikwepa  kulipa ushuru  huo .


Kwani  alisema kitendo cha  kushindwa kulipa ushuru  wa maegesho  ni sawa na kuhujumu uchumi wa Taifa  na hivyo suala  hilo halitavumilika hata  kidogo.


Wakati  mstahiki  meya  wa Halmashauri ya Manispaa ya  Iringa Aman Mwamwindi  mbali ya kuwashukuru  wajumbe wa kikao   hicho kwa kuipongeza Manispaa ya  Iringa kwa kufanya  vema bado alisema kuna  changamoto kubwa  ya madeni ya  walimu kiasi cha Tsh  bilioni 1.3  fedha ambazo  walimu hao  wanapaswa  kulipwa.


Huku  kuhusu  suala la ushuru  Mwamwindi alisema kuwa kuna tetesi   kuwa serikali inampango wa kufuta  ushuru  wa mazao  jambo ambalo ni hatari  zaidi katika uhai wa Halmashauri  za  wilaya katika kujiendesha .

0 comments: