Wakati
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akisema wabunge wa chama chake
watasusia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba ikiwa hoja ya kuundwa kwa
Serikali tatu itapingwa na wabunge wa CCM, Mwakilishi wa Mji Mkongwe
(CUF), Ismail Jussa Ladhu ametaka kuvunjwa kwa Muungano.
Akihutubia
kwenye Uwanja wa Tubuyu nje kidogo ya Mji wa Morogoro juzi, Mbowe
alisema wabunge wa chama chake wataandamana nchi nzima kufikisha ujumbe
kwa wananchi kwamba maoni yao yamepingwa na wabunge wa CCM walio wengi.
"Tutawaeleza
wananchi kwamba maoni ya CCM ndiyo yameonekana ya maana kuliko ya
wananchi ambao ni wengi zaidi," alisema Mbowe kwenye mkutano huo ambao
ni sehemu ya Operesheni ya Vuguvugu la Mabadiliko - M4C Pamoja Daima.
Alisema
Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilikusanya maoni na kubaini kuwa asilimia
62 ya Watanzania wanataka Serikali tatu za Tanganyika, Zanzibar na ya
Muungano.
"Serikali
ya CCM haitaki kusikia maneno Serikali tatu wanasema sera yao ni ya
Serikali mbili, wanafanya kila hila ili kuikataa hoja hiyo. Natangaza
kwamba wakifanya hivyo tutasusia na kwenda kuwashtaki kwa wananchi,"
alisema Mbowe.
Aliongeza kwamba wataandamana kuanzia Kagera hadi Mtwara kuwaeleza wananchi kwamba hoja yao imepingwa na CCM.
Mbowe
alisema baadhi ya viongozi wa CCM wamekuwa wakitoa kashfa dhidi ya
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kwamba
amechukua maoni ya Chadema.
"Wanakosea hayo si maoni ya Chadema, bali ni maoni ya wananchi, Warioba amezingatia maoni ya wananchi," alisema.
Mwenyekiti
huyo alisema Katiba inayotafutwa si ya chama, bali ni ya Watanzania na
kwamba inashangaza CCM kuipinga hoja Serikali tatu.
"Tunafahamu
wanaogopa kuikubali hoja ya Serikali tatu kwa sababu wanafahamu huo
ndiyo utakuwa mwisho wao wa kuwa madarakani," alisema Mbowe huku
akishangiliwa na wafuasi wa chama hicho.
Alisema
CCM wanaelewa kwamba kukiwa na Serikali tatu, Chadema kitashinda
Tanganyika na CUF Zanzibar katika uchaguzi wowote utakaoitishwa.
"Kwa hiyo
hivi sasa wana wasiwasi kweli, wanatafuta kila njia ya kuichakachua
hoja ya Serikali tatu lakini wafahamu kuwa Chadema wanaifuatilia hoja
hiyo kwa ukaribu," alisema.
Aliwataka
wananchi kufuatilia Bunge Maalumu la Katiba litakapoanza mwezi ujao ili
kuangalia wabunge wao wanavyowawalisha katika suala hilo muhimu.
Hata
hivyo, Mbowe alisema chama hicho kikishinda katika uchaguzi wa mwaka
2015 hakitahangaika kulipa kisasi kwa kuwachukulia hatua za kisheria
viongozi, bali kitajikita kutafuta maendeleo.
"Wasituogope
tutasamehe kama alivyosamehe aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Nelson
Mandela. Hatutalipa kisasi tukiingia Ikulu, kwa sababu hakuna binadamu
asiye na makosa. Tutaelekeza nguvu zetu kuwaletea maendeleo Watanzania,"
alisema Mbowe.
Jussa na Muungano
Akihutubia
mkutano wa kampeni katika Jimbo la Kiembesamaki jana, Jussa alisema
hakutakuwa na maendeleo yatakayofikiwa Zanzibar ikiwa Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar hautang'oka.
Jussa
ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa la CUF, alisema Zanzibar
yenye watu milioni 1.5 haiwezi kuwa na tatizo la watu kukosa ajira
lakini sera na mipango ya kiuchumi imekuwa ikikwama katika utekelezaji
wake kutokana na kukosa mamlaka kamili.
Alisema
Zanzibar haiwezi kukopa katika taasisi za kimataifa bila ya kuwekewa
dhamana na Waziri wa Fedha wa Muungano wakati Zanzibar ni nchi na
kuwataka wananchi kutumia kura zao katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 kuleta
mabadiliko ya kiutawala.
"Hakuna
sababu ya vijana Zanzibar kukosa ajira, kuna watu wasiozidi milioni 1.5,
Muungano umefika wakati ung'oke, ndiyo kikwazo cha maendeleo ya
Zanzibar na watu wake kiuchumi na kisiasa," alisema Jussa.
Alisema
mradi wowote unaobuniwa Zanzibar hauwezi kupata mfadhili bila kuwekewa
dhamana na Serikali ya Muungano na kukwama kwa juhudi zote za kujiunga
na jumuiya za kimataifa akitolea mfano Jumuiya ya Kimataifa ya Kiislamu
(OIC).
Alisema
Rais wa Zanzibar amepoteza mambo muhimu chini ya mfumo wa Muungano ikiwa
ni pamoja na kutopigiwa mizinga 21 akiwa nje ya nchi, kupeperusha
bendera ya Zanzibar, kutokagua gwaride na kupigiwa wimbo wa Taifa la
Zanzibar.
"Haya ya
sasa si mamlaka kamili, wapi Dk Shein alikokwenda akapigiwa mizinga 21
au alipeperushwa wapi bendera ya Zanzibar wakati wa safari zake za nje?"
alihoji Jussa.
0 comments:
Post a Comment