Monday, 27 January 2014

LIGI KUU ENGLAND-JUMANNE LEO MAN UNITED v CARDIFF, MATA, ROONEY & RVP NDANI! LIVERPOOL v EVERTON!

>>OLD TRAFFORD: MAN UNITED v CARDIFF, MATA, ROONEY & RVP NDANI!

>>VINARA ARSENAL UGENINI KWA ‘WATAKATIFU!’
LIGI KUU ENGLAND
BAADA KUPISHA FA CUP WIKIENDI, Ligi Kuu England inarejea dimbani Jumanne na Jumatano kwa Timu zote 20 kushuka Uwanjani.
ZIFUATAZO NI RIPOTI ZA VIKOSI/TATHMINI/RATIBA YA MECHI HIZO: BPL2013LOGO

RATIBA:
[Saa za Bongo]
Jumanne Januari 28
2245 Man United v Cardiff
2245 Norwich v Newcastle
2245 Southampton v Arsenal
2245 Swansea v Fulham
2300 Crystal Palace v Hull
2300 Liverpool v Everton

MAN UNITED v CARDIFF
MATA-NA_8Mchezaji mpya alievunja Rekodi ya kununuliwa kwa Dau la Bei mbaya, Juan Mata, anatarajiwa kuanza Mechi hii kwa Timu yake Manchester United itakapoikaribisha Cardiff City Uwanjani Old Trafford.
Ujio wa Mata ni habari njema kwa Man United ambao Wiki iliyopita walibwagwa nje ya Capital One Cup kwa Mikwaju ya Penati na Sunderland na Jumapili iliyopita walifungwa 3-1 na Chelsea huko Stamford Bridge kwenye Mechi ya Ligi.
Mwezi Novemba walipokutana huko Mjini Cardiff kwa mara ya kwanza tangu 1975, Man United na Cardiff City zilitoka Sare 2-2 na hivi sasa Cardiff wapo chini ya Meneja mpya Ole Gunnar Solskjaer ambae alikuwa Mchezaji Nguli hapo Old Trafford.
Katika Mechi yao ya mwisho ya Ligi, Cardiff walichapwa 4-2 na Man City huko Etihad na kujikuta wako mkiani kwenye Msimamo wa Ligi na kuendeleza mlolongo wao wa kutofanya vyema Mechi za Ugenini kwani wameshinda Mechi moja tu.
Man United inatarajiwa kuwa nao Mastraika wao Wayne Rooney na Robin van Persie ambao wamekuwa nje kitambo baada kupona maumivu yao lakini itawakosa Nahodha wao, Nemanja Vidic, ambae hii itakuwa Mechi ya Pili ya Kifungo chake cha Mechi 3 kufuatia Kadi Nyekundu aliyopewa kwenye Mechi na Chelsea, pamoja na Majeruhi Rio Ferdinand (Goti), Nani (Musuli ya Paja) na Michael Carrick (Enka).
Huenda Cardiff wakawa nae Mchezaji mpya Kenwyne Jones kutoka Stoke City ambae amebadilishana na Peter Odemwingie anaekwenda Stoke.
Pia, mpya mwingine kutoka Molde ya Norway, Jo Inge Berget, anaweza kuichezea Cardiff Mechi yake ya kwanza.
SOUTHAMPTON ARSENAL
LUKAS_PODOLSKI-ArsenalArsenal wanaweza kupanda Pointi 4 juu kileleni ikiwa wataifunga Southampton na kufikisha ushindi kwa Mechi 8 mfululizo.
Tangu wachapwe 6-3 na Man City Mwezi Desemba, Arsenal wameshinda Mechi 7 mfululizo na hawajafungwa na Southampton tangu Novemba 2002.
Staa wao Alex Oxlade-Chamberlain amerejea dimbani tena baada kukosekana kwa majeruhi tokea Agosti baada Juzi kucheza walipoitwanga Coventry Bao 4-0 kwenye FA CUP na pia Lukas Podolski, ambae pia alikuwa nje kwa muda baada kuumia, amerejea kwa kishindo na kwenye Mechi hiyo na Coventry alifunga Bao 2.
Arsenal bado itawakosa Majeruhi wa muda mrefu Abou Diaby na Theo Walcott, wote wakiwa na matatizo ya Goti.
Southampton, ambao wameshinda Mechi zao 3 zilizopita za Nyumbani, iatakuwa nao tena Majeruhi wao Rickie Lambert, Artur Boruc na Mkenya Victor Wanyama lakini itawakosa Pablo Daniel Osvaldo, aliefungiwa na Klabu baada kupigana Mazoezini, na Majeruhi Dejan Lovren na Gaston Ramirez.
SWANSEA v FULHAM
Swansea City wanaichungulia Mechi hii na Fulham kama nafasi ya kushinda baada kutoshinda katika Mechi 8 za Ligi.
Mwendo huo mbovu umeitupa Timu hiyo iliyo chini ya Meneja Michael Laudrup chini na wako Pointi 3 tu toka Timu 3 za mkiani wakati Mwezi Desemba walikuwa Pointi 8 juu yao.
Lakini nao Fulham, chini ya Meneja Rene Meulensteen ambae ni Kocha wa zamani wa Man United chini ya Sir Alex Ferguson, nao wako taabani hasa kwa Mechi za Ugenini ambazo mara ya mwisho kushinda ni Oktoba walipoichapa 4-1 Crystal Palace.
Tangu wakati huo, Fulham wamecheza Mechi 7 za Ugenini na kushinda moja tu na kufungwa Jumla ya Mabao 22 goals.
Lakini pia Swansea hawajashinda kwao Liberty Stadium katika Mechi 3 zilizopita ingawa hizo zilikuwa Mechi ngumu kwao dhidi ya Everton, Manchester City na Tottenham Hotspur.
Kwenye Mechi yao ya mwisho kati yao Mwezi Novemba, Swansea waliishinda Fulham Bao 2-1 huku Bao la ushindi likifungwa na Jonjo Shelvey katika Dakika 10 za mwisho lakini safari hii Jonjo yuko nje akijiuguza enka.

CRYSTAL PALACE v HULL CITY
Hull City wanasafiri kwenda kucheza na Crystal Palace huku wakitaka kukwepa kipigo cha 4 mfululizo kwenye Ligi.
Steve Bruce, Meneja wa Hull iliyo Nafasi ya 11, anatarajia kushinda ili kujinusuru kuburuzwa kwenye Timu za mkiani lakini wana rekodi mbaya Uwanjani Selhurst Park ambako hawajashinda katika Mechi 10 zilizopita kuanzia 1986.
Hull itamkosa Kiungo wao Tom Huddlestone ambae alipewa Kadi Nyekundu katika Mechi yao iliyopita na pia itawakosa Majeruhi James Chester, Joe Dudgeon na Sone Aluko.
Crystal Palace, chini ya Meneja Tony Pulis itawakosa Majeruhi Jack Hunt na Glenn Murray.

LIVERPOOL v EVERTON
ANFIELD_1Hii ni Dabi ya Merseyside, inayokutanisha Timu za Jiji la Liverpool Uwanjani Anfield, Liverpool v Everton, ambazo katika Dabi zao 3 zilizopita zote zilimalizika Sare ingawa Everton hajwashinda katika Dabi 7 zilizopita na mara ya mwisho ni Oktoba 2010.
Safari hii wanakutana huku Pointi 1 ikiwatenganesha kwenye Msimamo wa Ligi, Liverpool wakiwa Nafasi ya 4 na Everton Nafasi ya 6.
Katika Dabi yao ya mwisho, Mwezi Novemba huko Goodison Park, Daniel Sturridge alifunga Bao mwishoni na kuipa Liverpool Sare ya Bao 3-3.
Klabu hizi zina Mameneja wapya, Brendan Rodgers kwa Liverpool na Everton ni Roberto Martinez, na wote hawajawahi kuonja ushindi wa Dabi ya Merseyside.
Huku Liverpool wakiigeuza Anfield kuwa ngome yao, kwa kufungwa Mechi moja tu Mwezi Septemba Southampton waliposhinda 1-0, Everton wanakabiliwa na kibarua kigumu.
Kwa upande wa Majeruhi, Liverpool itawakosa Lucas Leiva (Goti), Jose Enrique (Goti) na Daniel Agger (Musuli za Mguu).
Everton watamkosa Mchezaji wao wa Costa Rica, Bryan Oviedo, ambae alivunjika Mguu mara mbili Juzi kwenye Mechi ya FA CUP na pia Majeruhi wengine Ross Barkley (Amevunjika Kidole cha Mguu), Darron Gibson na Arouna Kone (Wote Goti.)
Lakini Everton huenda wakamtumia Mchezaji wao mpya Lacina Traore.
LIGI KUU ENGLAND
RATIBA:
[Saa za Bongo]
Jumatano Januari 29
2245 Aston Villa v West Brom
2245 Chelsea v West Ham
2245 Sunderland v Stoke
2245 Tottenham v Man City

0 comments: