Na Thehabari.com
MTANDAO wa
Wanawake na Katiba wenye mashirika zaidi ya 50 yanayotetea haki za
wanawake katika Katiba mpya, umelipongeza mchakato na matokeo ya
uchaguzi wa kuwapata viongozi wa Bunge Maalum la Katiba (Mwenyekiti na
Makamu wake) ambao umezingatia usawa wa jinsia.
Kauli
hiyo imetolewa leo kwa vyombo vya habari na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji,
Lilian Liundi wa TGNP Mtandao kwa niaba ya Mtandao wa Wanawake na Katiba
jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa licha ya Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba, Sura ya 83 ya Mwaka 2012 haikuanisha kuwa uchaguzi wa uongozi wa
Bunge hili uzingatie usawa wa jinsia bunge hilo limeona umuhimu huo.
“…Tumetambua
busara na hekima za wajumbe za kuonyesha nia ya kujenga msingi wa usawa
wa jinsia katika uongozi na vyombo vya maamuzi nchini. Kwetu sisi, hili
si suala la uwepo wa mwanamume na mwanamke katika uenyeketi wa Bunge
Maalumu tu, bali pia ni ukomavu wa kipekee wa wajumbe katika kuuona
ukweli kuwa suala la kuimarisha sauti za wanawake na wanaume ni nyeti
sana, haswa wakati wa ujenzi wa maridhiano muhimu kikatiba,”
alisema Liundi.
“Tunawapongeza
waliochaguliwa ambao ni Mhe. Samweli Sitta (Mwenyekiti) na Mhe. Samia
Hassan Suluhu (Makamu Mwenyekiti) kwa kuaminiwa katika nyadhifa hizo
muhimu. Mtandao wa Wanawake na Katiba unatambua uwezo wao katika
utendaji na una matumaini makubwa kuwa pamoja na mengine mengi
watakayoyasimamia, watatoa uongozi ulio imara na wenye weledi wakati
wakiongoza Bunge hili katika kujadili na kupitisha misingi muhimu
itakoyopelekea katika ujenzi wa usawa wa kijinsia nchini.”
Alisema
mtandao huo unategemea kuona usawa wa jinsia ndani ya Katiba mpya,
ambao sio ule tu wa kuongeza ushiriki wa wanawake katika ngazi
mbalimbali, lakini pia usawa ulio na nia ya kujenga misingi ya kuleta
maendeleo ya kweli kwa wananchi walio wengi na haswa wanawake nchini.
“…Kwa
mtazamo huu, tunatarajia kuwa busara za Wenyeviti hawa na washauri wao
zitatumika pia kuzingatia usawa wa kijinsia katika Kamati zitakozoundwa
pamoja na kuwa kuzingatia ustadi na uzoefu wa wanakamati unahitajika.
Nia kubwa ikiwa kuona wanawake kwa wanaume watatoa sauti zao kuhakikisha
na kulinda, pamoja na mengine, uzingatiwaji wa usawa wa jjinsia katika
vifungu vyote vya Katiba mpya.”
Aidha
alifafanua kuwa Mtandao wa Wanawake na Katiba, unawapongeza wajumbe
wote wanawake kwa umoja wao, mshikamano na ushirikiano imara, ambao
umeleta mafanikio makubwa katika michakato inayoendelea huko Dodoma
kwenye Bunge Maalumu.
“…Huu
ni mwanzo wenye kuonyesha mifano mizuri, na ambao tunapenda kuuona
ukiendelezwa na kusimamiwa imara wakati wote Bunge Maalumu litakapokuwa
likifanya kazi yake ya kuchambua na kupitisha vifungu mbalimbali vya
Katiba,” alimalizia Bi. Liundi.
0 comments:
Post a Comment