Mtendaji
Mkuu Bodi ya Filamu, Bi. Joyce Fisoo akiwasilisha Rasimu ya awali ya
Sera ya Filamu wakati wa moja ya kikao cha wadau cha kujadili rasimu ya
awali ya Sera ya Filamu kilichofanyika hivi karibuni. Kulia ni
Mkurugenzi msaidizi kutoka Idara ya Sera na Mipango Wizara ya Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo, Bi. Verediana Mushi, na Kushoto ni mdau wa
filamu Bw. John Kitime.
Baadhi ya
wadau mbalimbali wa tasnia ya filamu wakijadiliana wakati wa kikao cha
wadau cha kujadili rasimu ya awali ya Sera ya Filamu kilichofanyika hivi
karibuni.
SERIKALI ya Tanzania
imejipanga kuendeleza kwa dhati tasnia ya filamu nchini ili kuwa chanzo
kikubwa cha ajira kwa wasanii na pia kuongeza uchumi wa nchi. Ni
dhahiri kuwa sekta ya filamu ni njia madhubuti ya kutambulisha jamii
kiutamaduni, kisiasa na kijamii na pia katika kukuza na kuongeza fursa
za nchi katika uwekezaji na utalii.
Filamu na makala za filamu zikitumika
vizuri zitaweza kuhamisha na kuondoa tofauti mbalimbali zilizopo ndani
ya jamii na hivyo kuongeza umoja na mshikamano baina ya watu wa makabila
na watu wenye asili mbalimbali, hivyo kuutambulisha utamaduni wa
Mtanzania. Kazi na shughuli za Filamu nchini zimekuwa zikisimamiwa na
Sera ya Utamaduni ambayo ilitayarishwa na kupitishwa mwaka 1997 pamoja
na Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza na 4 ya mwaka 1976.
Katika kipindi cha kuanzia mwaka 1997
hadi mwaka 2013 kumekuwepo na maendeleo makubwa katika Tasnia ya Filamu
nchini hivyo kuisababishia Sera ya Utamaduni ya Mwaka 1997 kutokidhi
baadhi ya mahitaji ya tasnia ya filamu na kupelekea mahitaji ya
kurekebisha Sera ya Utamaduni kama Sera mama na kutungwa kwa Sera ya Filamu.
Mnamo Desemba 12 mwaka 2013, wadau
mbalimbali kutoka Wizara ya Habari, Vijana Utamaduni na Michezo, Bodi ya
Filamu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Wizara ya Elimu
na Mafunzo ya Ufundi na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
walishiriki katika kikao cha wadau cha kujadili rasimu ya awali ya Sera
ya Filamu.
Wadau wengine ni Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii, Wizara ya Kazi na Ajira, BASATA, Idara ya Sanaa na
Sanaa za Maonesho, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mamlaka ya Mapato Tanzania, Mtandao wa Muziki, Swahili Films, ROSAF, TAPAF, Umoja wa Mashirikiano wa Filamu, Filamu Cental, Chama cha Hakimiliki Tanzania, Shirikisho la Sanaa za Maonyesho pamoja na G&S Associates and Advocates.
Wizara inapenda kuujulisha umma kuwa
imekua na inaendelea kushirikiana na wadau wa Filamu kwa kila hatua ili
hatimaye ifanikishe azma ya kuwa na nyaraka zote muhimu katika
kuendeleza, kusimamia, kuratibu na kukuza tasnia ya filamu nchini.
0 comments:
Post a Comment