Tuesday, 11 March 2014

MAHAKAMA YAVUNJA RASMI NDOA YA MFANYABIASHARA MKOANI SINGIDA


DSC07091
Jengo la mahakama ya mwanzo Utemini jimbo la Singida mjini.

Na Nathaniel Limu, Singida
MAHAKAMA ya mwanzo Utemini Mjini mjini hapa,  imeamuru kuvunjwa rasmi kwa ndoa na kutoa talaka dhidi ya mfanyabiashara Baltazar Mushi, maarufu kwa jina la Sammayuni (34) na mkewe Lucy Msuya (32), ili kuepusha udhalilishaji dhidi ya Mwanamke huyo.
Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Ferdnand Njau, ambaye pia mahakama hiyo iligawanya mali sawa, ili wanadoa hao kila mmoja anufaike na jasho lake katika ndoa hiyo iliyodumu kwa miaka sita na kujaliwa kupata watoto wawili.
Aidha makahama hiyo ilimwamuru mwanaume kuhakikisha kila mwezi anawasilisha mahakamani hapo Sh.100,000 kwa mtalaka wake, kwa ajili ya matunzo ya watoto wao wadogo wawili.
Pamoja na utetezi wa mfanyabiashara huyo kuwa anadaiwa deni kubwa linalofikia zaidi ya Sh. Milioni 200, Hakimu Njau amesema kuwa mume ataendelea kumiliki maduka mawili, stoo moja na nyumba moja iliyopo mtaa wa Unyankindi ili aendelee kulipa madeni hayo, ikiwa ni mgawanyo wa mali zao.

Pia katika Mgawanyo huo mahakama ilimpatia mume magari mawili madogo,masofa, vyombo vyote vya ndani vya kupikia, kiwanja cha Misuna na kiwanja kingine kilichopo jirani na kanisa la KKKT Usharika wa Immanuel Singida Mjini.
Aidha mahakama hiyo imegawa mali hizo kwa mke ambazo ni viwanja vitatu ikiwemo kiwanja ploti namba tisa mtaa wa Utemini,  kiwanja wa mtaa wa Semali na kiwanja kimoja kilichopo mkoani Dodoma.
Mali nyingine alizogawiwa mwanamke ni Runinga mbili na stendi zake, sabufa mbili. Hata hivyo baada ya hukumu hakimu Njau aliwaeleza wanadoa hao kuwa Wasiwe na ugomvi tena badala yake kila mmoja aendelee na mambo yake, kauli iliyojibiwa na Sammayuni kuwa, ‘nitaoa mke mwingine haraka’.
“Mheshimiwa hakimu, nitaoa mke mwingine haraka sana…tena mchumba mwenyewe yupo hapa hapa mahakamani ‘kicheko kwa watu waliohudhuria mahakama hiyo’,”amesema Sammayuni.

Katika shauri lililofunguliwa na mwanamke huyo hadi kufikia hatua ya kuomba talaka, ilidaiwa kuwa ndoa hiyo iliyofungwa juni 25,2006, mke amekuwa akipigwa na kudhalilishwa utu wake na mumewe tangu mwaka 2008, hali iliyochangia siku ya februari 16, 2013 aondoke kwenda kuishi jijini D’Salaam.

0 comments: