YANGA imeagiza kifaa maalumu nchini
Ujerumani cha kupima ufanisi wa wachezaji wake uwanjani ambacho
hakijawahi kuonekana kwenye ardhi ya Tanzania.
Kifaa hicho kidogo kinachopachikwa kwenye jezi ya
mchezaji upande wa nyuma, hutumika kwenye timu kubwa za Ulaya kutokana
na gharama zake na kwamba ni teknolojia ya kisasa zaidi ambayo inahitaji
umakini na utaalam.
Kocha wa Yanga, Hans Pluijm ameuagiza uongozi kuingiza nchini kifaa hicho kinachoitwa Vis
Track GPS. Kazi kubwa ya kipimo hicho ni kupima takwimu za ufanisi wa
mchezaji kuanzia mazoezini mpaka kwenye mechi ambazo zinaweza kusaidia
benchi la ufundi kujua kiundani afya, utendaji na ufiti wa mchezaji
husika.
Kipimo hicho pia kinapima umbali, mbio fupi za kasi na hata ulaji wa mchezaji.
Kwa mujibu wa wataalam ni kwamba kipimo hicho kinafichua kila kitu na hata kama mchezaji hayuko fiti kinamuumbua.
Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu Mkuu
wa Yanga, Beno Njovu alisema kocha ameusisitizia uongozi kwamba
anahitaji mashine hiyo maalumu ya kukusanya taarifa za wachezaji ili
kupandisha kiwango cha Yanga na kumrahisishia kazi.
"Tutamletea kocha mashine hizo,
nilishakwenda Ujerumani mwezi mmoja uliopita kwa lengo la kufuatilia na
tumeridhika nazo na sasa tunafanya mchakato wa mwisho kuzileta nchini
ili aanze kutumia,"alisema Ben
"Mashine hizi zitakuwa ni nafasi
nyingine kwa kocha kujua kila mchezaji anafanya nini kuanzia nidhamu ya
uwanjani, kuheshimu muda, mazoezi anafanya kwa uwezo gani, kwenye mechi
nako anajitumaje kulingana na majukumu aliyopewa na kocha, mwisho wa
mwezi taarifa hizo zinafanyiwa tathmini na kutoa majibu ya umuhimu wa
kila mchezaji,"alisisitiza kiongozi huyo.
Kiongozi huyo alisema baada ya ripoti
za mashine hizo kocha na benchi lake la ufundi litakaa na kujua mchezaji
gani wa kukaa naye na yupi wa kumuondoa.
Kwa mujibu wa wataalamu ambao ni madaktari kifaa hicho hakijawahi kutumia Tanzania.
Juma Sufian ambaye ni daktari wa Yanga
alisema: "Kifaa hicho ni kigeni kwa hapa nchini, hakuna timu ambayo
imewahi kutumia, kazi yake kubwa ni kupima uwezo wa mchezaji hasa viungo
katika kukimbia uwanjani kulingana na majukumu, vifaa hivyo vipo vya
aina mbalimbali vikitofautiana katika majukumu kidogo."
Mwanandi Mwankemwa ambaye ni daktari
mkongwe wa tiba kwa wanamichezo alisema: "Hizo ni mashine zinazotumika
kupima uwezo wa wachezaji katika kukimbia, kawaida mchezaji yeyote
tunategemea atakimbia kilomita 12 akiwa uwanjani, hilo utalipima kwa
kutumia kifaa kama hicho, vipo vya aina nyingi lakini mfano mzuri ni
kile ambacho kinatumiwa Ulaya kuweza kutoa taarifa ya mchezaji husika
amekimbia umbali gani utaliona hilo katika Ligi ya Mabingwa Ulaya,
kunakuwa na mashine maalum."
CHANZO:MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment