>>MALINZI AITAKIA HERI SIMBA MKUTANO MKUU WAO!
>>WATANZANIA WATANO WAKWAA UKAMISHNA CAF
>> SEMINA YA WAAMUZI YAANZA DAR
PATA RATIBA/TAARIFA ZA TFF:
VPL-LIGI KUU VODACOM
RATIBA:
Jumamosi Machi 15
Azam FC v Coastal Union
Mtibwa Sugar v Yanga
Kagera Sugar v Tanzania Prisons
Jumatano Machi 19
Yanga v Azam FC
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Machi 14, 2014
Klabu ya Simba itafanya mkutano wa wanachama wake Jumapili (Machi 16 mwaka huu) kwa ajili ya kuifanyia marekebisho Katiba yao.
Nachukua fursa hii kuwatakia kila la
kheri katika mkutano huo ambao ni muhimu katika kuhakikisha klabu yao
inapiga hatua katika maendeleo ya mpira wa miguu na ustawi wake kwa
ujumla.
Hata hivyo, nawakumbusha viongozi na
wanachama wa klabu ya Simba kuwa marekebisho hayo ni lazima yafanyike
kwa kuzingatia Katiba, Kanuni na maelekezo ya Shirikisho la Kimataifa la
Mpira wa Miguu (FIFA), Afrika (CAF) na Tanzania (TFF).
Aidha waraka wa TFF kwa wanachama wake wa Februari 7 mwaka huu uzingatiwe kikamilifu katika marekebisho hayo.
TFF inawatakia wanachama wa Simba
mkutano mwema, na inawakumbusha wazingatie umuhimu wa kudumisha amani na
maelewano katika klabu yao.
Jamal Malinzi
Rais
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Release No. 043
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Machi 14, 2014
SEMINA YA WAAMUZI YAANZA DAR
Semina ya siku mbili kwa waamuzi wenye
beji za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) na wale wa
ngazi ya juu nchini (elite) kwa robo ya kwanza ya mwaka huu inaanza
kesho (Machi 15 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Waamuzi na waamuzi wasaidizi 22 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wanashiriki katika semina hiyo ambayo pia itahusisha mtihani wa utimamu wa mwili (physical fitness test), na itamalizika keshokutwa (Machi 16 mwaka huu).
Baadhi ya waamuzi hao ni Charles Simon
kutoka Dodoma, Dalila Jafari (Zanzibar), Ferdinand Chacha (Mwanza),
Hamis Chang’walu (Dar es Salaam), Helen Mduma (Dar es Salaam), Israel
Mujuni (Dar es Salaam), Issa Vuai (Zanzibar), Janeth Balama (Iringa) na
Jesse Erasmo (Morogoro).
John Kanyenye (Mbeya), Jonesia Rukyaa
(Bukoba), Josephat Bulali (Zanzibar), Lulu Mushi (Dar es Salaam), Martin
Saanya (Morogoro), Mfaume Nassoro (Zanzibar), Mohamed Mkono (Tanga),
Mwanahija Makame (Zanzibar), Ngaza Kinduli (Zanzibar), Ramadhan Ibada
(Zanzibar) na Waziri Sheha (Zanzibar).
YANGA KUIVAA MTIBWA SUGAR VPL
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inaendelea
kesho (Machi 15 mwaka huu) kwa mechi tatu ambapo mabingwa watetezi Yanga
wataumana na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Nao vinara wa ligi hiyo, Azam
wanaikaribisha Coastal Union ya Tanga katika mechi itakayofanyika Uwanja
wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam.
Mechi nyingine itachezwa Uwanja wa
Kaitaba mjini Bukoba kwa kuwakutanisha wenyeji Kagera Sugar dhidi ya
maafande wa Tanzania Prisons kutoka jijini Mbeya.
WATANZANIA WATANO WAKWAA UKAMISHNA CAF
Watanzania watano wameteuliwa kuingia
kwenye jopo la makamishna watakaosimamia mechi mbalimbali za Shirikisho
la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kwa mwaka 2014 hadi 2016.
Kwa mujibu wa orodha iliyotumwa na CAF
kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Watanzania hao ni
Alfred Kishongole Rwiza wa Mwanza na Hafidh Ali Tahir wa Zanzibar ambao
wamerejeshwa tena kwenye jopo hilo.
Rwiza na Tahir ambao ni waamuzi wastaafu
wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) na wakufunzi wa
uamuzi walikuwepo kwenye jopo lililopita la 2012 hadi 2014.
Makamishna wapya kwa upande wa wanawake
ni Elizabeth Mwanguku Kalinga wa Mbeya na Isabellah Hussein Kapera wa
Dar es Salaam. Kamishna mwingine mpya kwa upande wa wanaume ni Muhsin
Ali Rajab kutoka Zanzibar.
Wakati huo huo, CAF imeandaa semina kwa makamishna wanaume itakayofanyika jijini Cairo, Misri kuanzia Aprili 3 hadi 4 mwaka huu.
Watoa mada kwenye semina hiyo ya siku
mbili ni Katibu Mkuu wa CAF, Hicham El Amrani, Mkurugenzi wa Mashindano
wa CAF, Shereen Arafa na Naibu Mkurugenzi wa Mashindano wa CAF, Khaled
Nassar.
Wengine ni Meneja wa Waamuzi wa CAF,
Eddy Maillet, Mkurugenzi wa Habari wa CAF, Junior Binyam, Mkurugenzi wa
Teknolojia ya Mawasiliano wa CAF, Tarek el Deeb na Mkurugenzi wa Masoko
na Televisheni wa CAF, Amr Shaheen.
Boniface Wambura Mgoyo
Media and Communications Officer
Tanzania Football Federation (TFF)
0 comments:
Post a Comment