MGOMBEA
Ubunge wa Jimbo la Chalinze kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),
Ridhiwani Kikwete ameahidi kuwa atajitahidi kutatua kero za maji, umeme
na ajira kwa vijana. Alisema hayo jana baada ya kuchukua fomu katika
ofisi za Msimamizi wa Uchaguzi wa Wilaya ya Bagamoyo, Shija Andrew.
Leo
anatarajia kurudisha fomu hiyo. Ridhiwani alipokuwa akienda kuchukua
fomu hiyo, alisindikizwa na mamia ya wanachama wa CCM wa majimbo ya
Chalinze na Bagamoyo, wakiwa wanaimba na kucheza kumshangilia mgombea
huyo.
Baada ya
kuchukua fomu kutoka kwa Ridhiwani alimhakikishia ofisa huyo kuwa
atazingatia taratibu zote za uchaguzi na kutoendesha kampeni za matusi
na vurugu.
Baada ya
kuchukua fomu hiyo na nakala nyingine muhimu za uchaguzi, aliongozana
tena na mamia ya wafuasi wake, kuelekea kwenye ofisi za CCM Wilaya ya
Bagamoyo, ambapo alizungumza na waandishi wa habari.
Katika
mazungumzo yake hayo, Ridhiwani alitaja vipaumbele vyake kwa kuleta
maendeleo kwa wakazi wa Chalinze. Alisisitiza kuimarisha upatikanaji wa
maji salama na ya uhakika, kuimarisha afya, elimu na kukuza ajira kwa
vijana.
"Kama
mnavyofahamu kuwa Chalinze ni eneo ambalo linakabiliwa na changamoto
nyingi kama vile maji, umeme na hata suala zima la ajira kwa vijana,
sasa pindi nikipata Ubunge kwangu mimi nitahakikisha kuwa napunguza kama
sio kumaliza kabisa tatizo hilo," alisema Ridhiwani.
Aliongeza
kuwa "Mimi nimeguswa na changamoto mbalimbali zinazowakuta wakazi wa
wilaya hii na kama ambavyo nilisema kuwa sikushinikizwa, ila ni kwa
matakwa yangu mwenyewe, naona kabisa kuwa nipo katika hali na nguvu ya
kushirikiana na wakazi hawa kumaliza shida za Chalinze".
Ridhiwani pia alisema kuwa atasaidia kutatua ugomvi wa mara kwa mara, unaowakumba wakulima na wafugaji na kuwataka wakazi wa Chalinze kumchagua.
Wakati
huo huo, mgombea wa Ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chama cha
Demokrasia na Maendeleo, Matayo Torongey alisema kuwa anavyo vipaumbele
vingi na kimojawapo ni kuinua maisha ya wakazi wa Chalinze.
Alisema
hayo baada ya kuchukua fomu. Kipaumbele chake kingine kutatua tatizo la
ajira kwa vijana wa Chalinze na pia kupambana na umasikini.
Tongorey
alisema pia kuwa atajitahidi kutatua kero za maji, barabara na umeme
katika jimbo hilo. Alisema yeye analijua vema jimbo hilo na aliomba
wananchi wamchague siku ya kupiga kura.
Mgombea Ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Alliance For Tanzania Farmers
Party (AFP), Ramadhan Mgaya, akizungumza baada ya kuchukua fomu,
alisema atajitahidi kuinua kilimo na ufugaji katika kukuza maisha ya
wakazi wa Jimbo la Chalinze.
Wagombea wa AFP na Chadema walipokutana, wakati wakichukua fomu hizo, walianza kutaniana, ambapo Ramadhan Mgaya wa AFP alimwambia mgombea wa Chadema, Matayo Torongey kuwa ataongoza Ubunge huo na kisha kumwachia nafasi ya pili Matayo.
Matayo alionekana kushangaa vazi la Mgaya wa AFP, kuwa linafanana na lile la Chadema.
Alimtaka
mgombea huyo wa AFP, kujiunga na Chadema ili waweze kuchukua jimbo hilo.
Uchaguzi wa jimbo la Chalinze unafanyika, kufuatia kifo cha aliyekuwa
Mbunge wa Jimbo hilo, Saidi Bwanamdogo aliyefariki Januari 22 mwaka huu.
CHANZO:HABARILEO
0 comments:
Post a Comment