Wednesday, 12 March 2014

MENEJA NEWCASTLE, ALAN PARDEW, KIFUNGO MECHI 7!!

>>KIFUNGO: MECHI 3 ZA KWANZA, MARUFUKU UWANJANI, 4 KUTOKAA BENCHI!!
>>NI MARA YA KWANZA MENEJA KUFUNGIWA KUTOKANYAGA UWANJANI!
PARDEW-NDONGAMENEJA wa Newcastle United Alan Pardew amefungiwa Mechi 7 kwa kumpiga Kichwa Mchezaji wa Hull City, David Meyler, wakati wa Mechi ya Ligi Kuu England, na hii ni Rekodi mpya kwa upande wa Mameneja.
Tukio hilo lilitokea hapo Machi Machi 1 kwenye Dakika ya 72 katika Mechi ya Ligi ambayo Newcastle waliifunga Hull City Bao 4-1 na Pardew kutolewa kwenye Benchi na kuamriwa kukaa Jukwaani huku Meyler akipewa Kadi ya Njano.
Jopo Huru la FA, Chama cha Soka England, kimemfungia Pardew Jumla ya Mechi 7 huku 3 za kwanza akiwa haruhusiwi kukanyaga Uwanjani na 4 za mwisho hataruhusiwa kukaa Benchi.
Hii ni mara ya kwanza kwa Meneja kufungiwa asikanyage Uwanja wa Soka.
Vile vile, Pardew, mwenye Miaka 52, ametwangwa Faini ya Pauni 60,000 na kupewa Onyo kuhusu mwenendo wake wa baadae.
Mara baada ya tukio hilo la kumpiga Kichwa David Meyler, Klabu yake, Newcastle ilimwadhibu Pardew kwa kumpiga Faini £100,000 na kumpa Onyo rasmi.
Mwaka 2012, Pardew alifungiwa Mechi 2 kwa kumsukuma Msaidizi wa Refa na pia anayo matukio kadhaa ya mifarakano.

Mwezi Januari, ilibidi aombe radhi baada ya kunaswa akimkashifu Meneja wa Man City, Manuel Pellegrini, wakati wa Mechi Uwanjani Saint James Park ambayo Newcastle ilifungwa 2-0 na Man City.
Novemba 2006, alimwomba radhi Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, kwa kushangilia kupita kiasi mbele ya Wenger baada ya Newcastle kufunga Bao la Ushindi walipocheza na Arsenal na hili tukio lilikuja Miezi 8 baada ya Wenger kumtuhumu ni ‘Mbaguzi.’

0 comments: