Jumla ya
Walimu wapya 36,021 ambao wamehitimu mwaka 2013 kutoka vyuo mbalimbali
hapa nchini wataajiriwa rasmi na Mamlaka za Serikali za Mitaa
(Halmashauri) ifikapo tarehe 01 Aprili 2014. Kati ya idadi hiyo walimu
wa ngazi ya Cheti (Daraja III A) ambao hufundisha katika shule za Msingi
ni 17,928 na walimu wa shule za sekondari ni 18,093 (wakiwemo 5,416 wa
Stashahada na 12,677 wenye shahada).
Orodha rasmi ya walimu wapya ikionesha
Halmashauri mbalimbali walikopangwa itatangazwa kwenye tovuti ya Ofisi
ya Waziri Mkuu TAMISEMI (www.pmoralg.go.tz) na ya Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi (www.moe.go.tz) ifikapo tarehe 15 Machi, 2014.
Walimu wote wapya wanatakiwa kuripoti
bila kukosa kwenye Halmashauri walikopangiwa ifikapo tarehe 01 Aprili,
2014 ili waanze kazi mara moja.
Inasisitizwa kwamba walimu waripoti
tarehe hiyo ili taarifa zao za kiutumishi zifanyiwe kazi na Waajiri wao
yaani Wakurugenzi ili kuwawezesha kupata mshahara mwezi Aprili 2014 na
hivyo kuepuka ulimbikizaji wa mshahara kwa watumishi wapya wanaoanza
ajira.
Mwalimu yoyote ambaye ataripoti baada
ya tarehe 10 Aprili, 2014 bila sababu za msingi zinazokubalika
kiutumishi atakuwa amepoteza nafasi hiyo.
Ikumbukwe kwamba Upangaji wa Walimu
wapya kwenye Halmashauri umezingatia uwepo wa mahitaji ya walimu. Vile
vile, fedha za kujikimu kwa muda wa siku saba na nauli ambazo zitalipwa
kwa kila mwalimu atakayeripoti kulingana na viwango vilivyowekwa na
Serikali zimetumwa kwenye Halmashauri walikopangwa walimu hao. Hivyo,
kila mwalimu anatakiwa kwenda kuripoti katika Halmashauri alikopangwa.
Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI
haitafanya mabadiliko yoyote ya vituo vya kufanya kazi walimu wapya
isipokuwa kwa utaratibu wa kawaida wa uhamisho baada ya mwalimu kutimiza
vigezo na masharti ya uhamisho.
Ni vema ifahamike kuwa ajira
zinazotangazwa ni za walimu wapya. Walimu ambao tayari ni watumishi umma
waliokuwa vyuoni kwa ajili ya kujiendeleza kielimu na hivi sasa
wamehitimu mafunzo yao, wanatakiwa kurudi kwa waajiri wao na kuendelea
na kazi.
Ofisi ya waziri mkuu- TAMISEMI.
0 comments:
Post a Comment