Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha Waziri wa
Fedha, Mheshimiwa William Mgimwa, aliyekuwa pia Mbunge wa Jimbo la
Kalenga (Mkoa wa Iringa) kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM).
Rais
Kikwete amesema kuwa taifa limempoteza Waziri Mgimwa katika kipindi
lilipokuwa linamhitaji zaidi kutokana na mchango wake mkubwa ambao
amekuwa akiutoa kupitia nafasi zake za Waziri wa Serikali na mwakilishi
wa wananchi wa Jimbo la Kalenga.
Kifo cha
Mheshimiwa Mgimwa kimetangazwa mchana wa leo, Jumatano, Januari Mosi,
2014, na Katibu Mkuu Kiongozi (KMK) Balozi Ombeni Sefue kwa niaba ya
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika
tangazo lake, Balozi Sefue amesema kuwa Waziri Mgimwa ameaga dunia
asubuhi ya leo saa 5:20 (Saa za Afrika ya Kati) katika Hospitali ya
Kloof Medi-Clinic , Pretoria, Afrika Kusini ambako amekuwa amelazwa kwa
muda sasa.
Balozi
Sefue amesema kuwa maandalizi ya kuurudisha nyumbani mwili wa Waziri
Mgimwa yanafanywa na Serikali kwa kushirikiana na familia yake na kuwa
taarifa zaidi kuhusu suala hilo zitatolewa baadaye kwa kadri
zinavyopatikana na maandalizi yanavyoendelea.
Katika salamu zake kwa Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda na kwa familia ya Marehemu Mgimwa, Rais Kikwete amesema: “Sina
maneno ya kutosha kuelezea mshtuko na huzuni yangu kubwa kufuatia
taarifa za kifo cha Mheshimiwa Mgimwa. Binafsi nimemtembelea mara mbili
kwenye Hospitali alikokuwa amelazwa na mara ya mwisho hali yake ilikuwa
imeimarika. Tulizungumza kwa kiasi cha dakika 10 hivi akanielezea nia
yake na tamaa yake ya kurejea nyumbani kwa sababu hali yake ilikuwa
nzuri.”
Ameongeza Mheshimiwa Rais Kikwete: “Sote tunajua mchango wake katika Serikali. Sote tulitamani kuendelea kuwa naye, lakini haya ni mapenzi ya Mungu.”
“Napenda
kutoa pole nyingi na rambirambi zangu za dhati kwa wana-familia wote
kwa kuondokewa na mhimili wao. Naungana nanyi katika kuomboleza msiba
huo mkubwa. Napenda mjue kuwa msiba huu ni msiba wangu pia. Machungu
yenu ni majonzi yangu,” amesema Rais Kikwete.
Rais pia
amewatumia rambirambi wananchi wa Jimbo la Kalenga akisema kuwa
wamempoteza mwakilishi na mtetezi mahiri wa maslahi yao.
0 comments:
Post a Comment