Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akikagua Daraja la Mto Mkundi mkoani Morogoro linalokarabatiwa baada ya kuharibiwa na mafuriko hivi karibuni.Rais Kikwete alitembelea eneo hilo na sehemu nyingine zilizokumbwa na mafuriko hayo kujionea uharibifu(picha na Freddy Maro)
Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akikagua Daraja la Mto Mkundi mkoani Morogoro linalokarabatiwa baada ya kuharibiwa na mafuriko hivi karibuni.Rais Kikwete alitembelea eneo hilo na sehemu nyingine zilizokumbwa na mafuriko hayo kujionea uharibifu(picha na Freddy Maro)
……………………………………………………………………………..
Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi la Ulinzi na
Usalama, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameliamuru Jeshi la Wananchi
wa Tanzania (JWTZ) kuanza mara moja kazi ya kusimamia utoaji huduma kwa
watu walioathiriwa na mafuriko katika Mkoa wa Morogoro, ikiwa ni pamoja
na kusimamia ujenzi wa nyumba za muda wa wahanga hao.
Rais
pia ameliamuru Jeshi kupeleka mashine za kusafisha maji katika makambi
ambako wahanga hao wa mafuriko ya Januari 22, mwaka huu wanaishi kwa
muda.
Aidha,
Rais Kikwete amewahakikishia wahanga wa mafuriko hayo kuwa Serikali
itahakikisha inawapatia huduma zote za msingi ikiwa ni pamoja na
chakula, malazi, maji na huduma za afya hadi hapo watakapokuwa na uwezo
wa kuanza kujitegemea tena.
Rais
Kikwete ametoa amri hizo kwa Jeshi leo, Januari 27, 2014, wakati
alipotembelea kambi za wahanga wa mafuriko hayo kuwajulia hali
walioathirika katika makambi yaliyoko Shule ya Sekondari ya Magole
katika eneo la Dumila na katika Kijiji cha Mateteni kilichoko Dakawa,
Wilaya ya Kilosa.
Katika
hotuba zake fupi baada ya kuwa ametembelea na kuona mahema ambamo
wahanga hao wanalala, Rais Kikwete amesema ameagiza Jeshi kuongoza
harakati za kuwahudumia wahanga hao kwa sababu zikifuatwa taratibu za
kawaida za Kiserikali huduma zitachelewa sana kuwafia waathirika.
“Kazi
yetu ni kusimamia maisha ya watu hasa kipindi cha shida za namna hii.
Tukifuata taratibu za kawaida za Kiserikali za tenda tutachelewesha
sana huduma za dharura kwa waathirika. Ndiyo maana nimeliamuru Jeshi
kufanya kazi hii ikiwa ni pamoja na kujenga haraka makazi ya muda wa
waathirika,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Katika
mazungumzo hayo na Mkuu wa Majeshi, nimemwagiza pia kuleta mashine za
kusafishia maji ili kuhakikisha kuwa watu wanakunywa maji salama kwa
sababu katika hali ya sasa maji yasiyokuwa salama yanaweza kuwa chanzo
cha magonjwa.”
Kuhusu
upatikanaji wa chakula cha msaada kwa wahanga, Rais Kikwete amesema
kuwa Serikali inacho chakula cha kutosha kwa ajili yao. “Tunacho chakula
cha kutosha na hata kile tusichokuwa nacho tutanunua. Tutabanana ndani
ya Serikali ili tupate fedha za kutosha za kuwahudumia.”
Kuhusu
malazi, Rais amesema:”Naambiwa kuna upungufu wa magodoro. Tutahakikisha
kuwa yanapatikana na yatafika katika siku mbili zijazo. Hatutaki watu
walale chini na waje kupata vichomi.”
Kuhusu maji, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali itaendelea kutoa huduma
ya maji bure kwa wahanga. “Tutaendelea kutoa bure huduma hii mpaka hapo
huduma ya kawaida ya maji itakapoanza kupatikana tena.”
Kuhusu
huduma za afya, Rais amesema kuwa anafurahi kuwa kila kambi ya wahanga
inayo huduma ya afya ambayo itaendelea kutolewa kwa kadri watu
wanavyozidi kuishi kwenye makambi.
Rais
ameagiza kuwa baada ya muda mfupi viongozi wa Mkoa wa Morogoro na
wilaya husika wakae chini ya viongozi wa ngazi za chini na wahanga
kujadili na kutafuta mwafaka kuhusu maisha ya baadaye ya wahanga – hasa
kuhusu namna gani wanaweza kupatiwa maeneo yaliyoko nje ya mikondo ya
mafuriko.
“Hili ni lazima kwa sababu hata kama imechukua miaka mingi kwa
mafuriko ya sasa kutokea ni dhahiri kuwa iko siku yatakuja tena –
inaweza kuwa hata mwaka huu kwa sababu zipo mvua za masika. Kwa hiyo ni
lazima tukubaliane jinsi gani ya kurudi ama kutokurudi katika maeneo
yetu tulikotoka.”
0 comments:
Post a Comment