Mbunge wa Nzega (CCM), Dk Hamis Kigwangalla akichangia jambo bungeni siku za hivi karibuni mjini Dodoma. Picha na Maktaba
Dar es Salaam. Mbunge wa Nzega
(CCM), Dk Hamis Kigwangalla yuko hatarini kuvuliwa uanachama wa chama
hicho, hatua ambayo endapo itachukuliwa itasababisha apoteze nafasi yake
ya ubunge.
Uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya
Nzega mkoani Tabora tayari umemjadili Dk Kigwangalla katika vikao vyake
vya Kamati za Usalama na Maadili na Kamati ya Siasa, kuhusu kile
kinachodaiwa kuwa ni utovu wa nidhamu wa mbunge huyo.
Habari zilizolifikia gazeti hili jana jioni
zinasema baada ya vikao hivyo vilivyofanyika Januari 11 mwaka huu,
imeazimiwa kuwa suala la Dk Kigwangalla pamoja na madiwani watano
wilayani humo lipelekwe katika ngazi ya CCM mkoa na baadaye taifa.
Dk Kigwangalla jana alipotafutwa kuzungumzia suala
hilo alisema: “Hata mimi nimesikia taarifa hizo, isipokuwa sijapewa
taarifa rasmi. Ila nafahamu kwamba vikao vya chama vilikuwepo na mimi
niliitwa ila kama ambavyo nimeshasema siwezi kuhudhuria”.
Gazeti hili lilimtafuta Mbunge huyo machachari
kutokana na taarifa yake aliyoitoa kwenye mitandao ya Facebook na
Tweeter akieleza kuhusu taarifa za kuwapo mpango wa kumfukuza uanachama.
Kupitia mitandao hiyo Dk Kigangwalla aliandika:
“Nimepokea taarifa kuwa madiwani walioungana na wananchi wa Nzega pamoja
na mimi kupinga uamuzi wa Baraza la Madiwani kuzigawa pesa kwenye Kata
wameadhibiwa na Kamati ya Siasa ya Chama Wilaya ya Nzega, bila
kusikilizwa na ilhali miongoni mwa ‘mahakimu’ hawa ni watu waliokuwa
wakilalamikiwa na madiwani na wananchi. “
Mbunge huyo aliongeza: “Nimepewa taarifa kuwa
mapendekezo ya adhabu dhidi yangu kutoka wilayani kwenda vikao vya juu,
...tena bila kusikilizwa maana nilitoa udhuru, ni kuwa ninyang’anywe
kadi ya uanachama wa CCM. Nimeshangazwa sana na kusikitishwa na jinsi
chama kinavyoendeshwa Nzega.”
Mbunge huyo alisema anaamini viongozi wakuu wa CCM
wanafuatilia kwa karibu suala hilo na watachukua hatua stahiki, huku
akisema hatahudhuria tena kikao chochote cha CCM wilayani humo.
“Kama chama hiki kimefika huku, kwamba kuna watu
wana nguvu kuliko chama, kwamba wachache wanaweza kuwaonea wengine kwa
kuwa wana vyeo na mamlaka ya kufanya hivyo na hakuna wa kuingilia kati
na kusema ‘no’, basi sina haja ya kuendelea kupambana,” aliongeza.
Aliendelea: “Nimechoka, sintokata rufaa wala
sintolalamika tena. Watekeleze hukumu hiyo. Sintojitetea na
sintohudhuria kikao chochote kile kuanzia sasa, nimechoka kupambana na
watu wenye nguvu, nimechoka. Ni bora kuwa mnyonge, lakini ukabaki na
uhai, uzima, heshima na furaha yako”
.Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
0 comments:
Post a Comment