>>KLABU ZATAKIWA KUREKEBISHA KASORO USAJILI MDOGO
>>PAN AFRICAN WATAKIWA KUFUATA NGAZI HUSIKA
>>WATAKIWA KUHESHIMU UAMUZI WA TPLB
SOMA ZAIDI:
Release No. 216
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Desemba 29, 2013
KLABU ZATAKIWA KUREKEBISHA KASORO USAJILI MDOGO
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji
ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imekutana Jumamosi
(Desemba 28, 2013) kujadili mambo mbalimbali yaliyofikishwa mbele yake
ikiwemo usajili wa dirisha dogo ambapo klabu zenye matatizo zimepewa
hadi Januari 10 mwakani kurekebisha.
Baadhi ya klabu ikiwemo Simba
zimezidisha idadi ya wachezaji, hivyo zimepewa hadi muda huo kupunguza
ambapo zikishindwa kazi hiyo itafanywa na Kamati yenyewe.
Simba ina nafasi tano za kujaza kwenye dirisha dogo lakini imewasilisha majina ya wachezaji sita.
Pia klabu nyingine zimetakiwa ama
kuvunja mikataba ya wachezaji au kuendelea kuwa nao, na si kuendelea
kuwalipa mishahara wakati imeshawaondoa katika orodha yao.
RAGE BADO MWENYEKITI HALALI SIMBA
Ismail Aden Rage ndiye Mwenyekiti halali
wa Simba ambapo Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji imemtaka
kuitisha Mkutano Mkuu kwa mujibu wa taratibu za klabu ya Simba.
Kamati imebaini upungufu kadhaa wa
kisheria kwenye uamuzi wa Kamati ya Utendaji ya Simba uliofanywa Novemba
18, 2013 kwa kumsimamisha Mwenyekiti wao. Upungufu huo ni pamoja na
ukiukwaji wa Ibara ya 33 ya Katiba ya Simba juu uitishaji wa mkutano,
ajenda ya kumsimamisha Mwenyekiti kuwasilishwa kwenye kikao kwa
utaratibu wa mengineyo.
Changamoto nyingi zilizoelekezwa kwa Mwenyekiti huyo zingeweza kupatiwa ufumbuzi kwa kutumia Ibara ya 16(2) ya Katiba ya Simba.
Hivyo, agizo za Rais wa TFF, Jamal
Malinzi kumtaka Mwenyekiti wa Simba aitishe mkutano lipo palepale. Pia
Mwenyekiti ametakiwa kufanya uchaguzi wa kujaza nafasi ya Makamu
Mwenyekiti kwa kuzingatia Katiba ya klabu hiyo.
Katika mkutano huo wa kujaza nafasi,
ndiyo utakaojadili mgogoro kati ya Mwenyekiti na Kamati yake ya
Utendaji. Nafasi hiyo kwa sasa inakaimiwa na mjumbe wa Kamati ya
Utendaji ya klabu hiyo, Joseph Itang’are baada ya Geofrey Nyange
aliyekuwa akiishikilia kujiuzulu.
TFF inakumbusha wanachama wake wote
(vyama vya mikoa, vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu) kuzingatia Katiba
zao. Kamati pia imegundua ukikwaji wa maadili katika suala hili, hivyo,
litapelekwa katika kamati husika.
Kwa vile maslahi ya TFF ni kuona mpira wa miguu unachezwa kwa utulivu, itazikutanisha pande husika wakati wowote kuanzia sasa.
Kuhusu mchezaji Emmanuel Okwi ambaye
aliuzwa nchini Tunisia, TFF inafahamu kuwa klabu ya Simba bado
haijalipwa na itasaidia kufuatilia FIFA fedha za mauzo ya mchezaji huyo.
AJENDA, MUHTASARI WA KUMNG’OA KATIBU COREFA ZATAKIWA
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji
ya TFF imekitaka Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA)
kuwasilisha ajenda na muhtasari wa vikao vilivyofanya uamuzi wa kumvua
madaraka Katibu wake Riziki Majalla.
Ajenda na muhtasari unaotakiwa ni wa
vikao vya Kamati ya Utendaji iliyomsimamisha Katibu huyo kutokana na
tuhuma mbalimbali dhidi yake, na Mkutano Mkuu ambao ulimvua madaraka.
WATAKIWA KUHESHIMU UAMUZI WA TPLB
Wanachama wa Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) wametakiwa kuheshimu uamuzi halali unaofanywa na
vyombo vyake kwa kuzingatia katiba na kanuni zake.
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji
ya TFF imetoa maelekezo hayo baada ya klabu ya Stand United kukata
rufani kupinga uamuzi wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kuagiza mechi
yao ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) dhidi ya Kanembwa JKT iliyovunjika
kurudiwa Februari Mosi mwakani mjini Tabora.
Sekretarieti ya TFF iliwasilisha suala
hilo kwa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ili itoe mwongozo kwa
vile uamuzi huo uliofanywa na TPLB hauwezi kukatiwa rufani kwa mujibu wa
Kanuni za ligi husika.
Kamati imesisitiza kuwa hiyo ni falsafa
ya mpira wa miguu ambapo uamuzi unaofanywa uwanjani haukatiwi rufani,
hivyo uheshimiwe kama ilivyo kwa masuala ya mpira wa miguu kutopelekwa
katika mahakama za kawaida za kisheria.
PAN AFRICAN WATAKIWA KUFUATA NGAZI HUSIKA
Wanachama wa Pan African wametakiwa kufuata ngazi husika pale wanapoona viongozi wa klabu yao wanakwenda kinyume na Katiba yao.
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji
imetoa mwongozo huo kwa wanachama wa Pan African baada ya kumwandikia
barua Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
kulalamikia uongozi wao wakati wao si wanachama wa TFF.
Wanachama hao wanalalamikia uongozi wa
klabu yao kwa kuitisha mkutano wa uchaguzi kabla ya ule wa kawaida ambao
unatakiwa kufanyika mara moja kwa mwaka.
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji
ya TFF imelazimika kutoa mwongozo huo kwa vile wanachama hao katika
malalamiko yao wamekigusa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam
(DRFA) ambacho ni mwanachama wa TFF.
Pan African ni mwanachama wa Chama cha
Mpira wa Miguu Wilaya ya Ilala (IDFA) ambao ndiyo wanachama wa DRFA.
Hivyo, TFF imemtaka mwanachama wake DRFA kupitia IDFA kufuatilia tatizo
hilo na kulipatia ufumbuzi.
MKUTANO WA WAANDISHI JB BELMONTE
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) limeitisha Mkutano na Waandishi wa Habari utakaofanyika Jumanne
(Desemba 31, 2013) saa 6 kamili mchana.
Mkutano huo utafanyika kwenye hoteli ya JB Belmonte iliyoko Jengo la NSSF Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Boniface Wambura Mgoyo
Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 comments:
Post a Comment