Friday, 27 December 2013

MKWASA: NAJIAMINI, NDIYO MAANA NIMEKUBALI KURUDI YANGA

 
Najiamini; Charles Boniface Mkwasa amesema anajiamini ndiyo maana amekubali kazi Yanga
Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
KOCHA Mkuu wa Ruvu Shooting, Charles Boniface Mkwasa amekubali kushuka cheo hadi kuwa Kocha Msaidizi wa klabu ya Yanga SC ya Dar es Salaam na wakati wowote atasaini Mkataba wa kuanza kazi Jangwani.
Mkwasa aliiongoza kwa mara ya mwisho Ruvu Shooting jana ikifungwa mabao 3-0 na Azam FC katika mchezo wa kirafiki, Uwanja wa Azam Complex na baada ya mechi hiyo akasema; "Kweli, niko njiani kurejea Yanga, lakini bado sijasaini Mkataba, tumefikia makubaliano tu,"alisema kiungo huyo wa zamani wa kimataifa wa Tanzania.

Mkwasa amesema makocha wengi wa Tanzania kwa sasa wanaogopa kufanya kazi timu za Simba na Yanga kutokana na desturi ya kufukuza walimu ovyo, lakini yeye anajiamini atafanya kazi nzuri ambayo itamuepushia ‘balaa’ la kutupiwa virago.
“Mimi ni mwalimu ambaye najiamini, naweza kufanya kazi sehemu yoyote wakati wowote, hii Yanga SC mimi nimekwishafanya kazi kwa mafanikio kama mchezaji na kama kocha pia, sina wasiwasi wowote,”alisema Mkwasa maarufu kama Master enzi zake anatamba katika safu ya kiungo.
Charles Boniface Mkwasa aliyezaliwa Aprili 10, mwaka 1955 mjini Morogoro alijiunga na Yanga SC kwa mara ya kwanza kama mchezaji mwaka 1978 akitokea Tumbaku ya Morogoro na akacheza hadi 1988 alipostaafu na kwenda kuanza maisha ya ukocha katika klabu ya Super Star ya Dar es Salaam mwaka 1989.

Imetumwa kwenye Michezo
Soma zaidi...

0 comments: