Sunday, 29 December 2013

TANZANIA NA KENYA ZASHIRIKIANA KUTHIBITI UJANGILI

 
Hifadhi Jamii ya Wanyama (WMA) la Enduimet, Wilayani Longido

Wadau wa uhifadhi wanyama pori kati ya Tanzania na Kenya wameanzisha ushirikiano wa kudhibiti ujangili wa wanyama pori katika mpaka wa kaskazini mwa Tanzania.

Ushirikiano huo unahusisha kubadilishana taarifa za kihalifu, intelijensia na kufanya doria za pamoja katika mapito ya wanyama pori eneo hilo ambalo linaunganisha hifadhi za Arusha, Kilimanjaro na hifadhi ya Amboseli ya Kenya

Wakizungumza katika mkutano wa pamoja uliofanyika katika eneo la Hifadhi Jamii ya Wanyama (WMA) la Enduimet Wilayani Longido, walisema uwindaji wa tembo na simba katika eneo la mpaka limekuwa ni tatizo kubwa.

Mkuu wa usalama katika eneo la hifadhi jamii la Enduimet, Imanuel Bujiku, alisema wawindaji wamekuwa wakiwinda wanyama na kukimbilia nchi jirani kukimbia kukamatwa.

Bujiku alisema ushirikiano huo umehusisha idara zote za ulinzi usalama katika nchi zote zikiwemo polisi na vikosi vya kudhibiti ujangili.

“Lengo kuu la ushirikiano wetu ni wa kuhakikisha eneo la mapito ya wanyama kutoka Hifadhi ya Amboseli Kenya kuja Tanzania tunaweka ulinzi wa kutosha kuzuia mauaji ya wanyama,” alisema Bujiku.


Kuhusu hali ya ujangili katika eneo la Enduimet, alisema kuanzia Januari hadi Oktoba, ya majangili 16 walikamatwa pamoja na gari moja, baiskeli nane pikipiki tano na watuhumiwa kufikishwa mahakakani.


Mhifadhi jamii kutoka Hifadhi ya Amboseli Kenya, Francis Irungu, alisema ushirikiano huo utadhibiti ujangili na kuleta tija kubwa katka uhifadhi wanyama pori.


Samwel Ole Kaangi kutoka mfuko wa uhifadhi wa Big Life nchini Kenya, alisema ushirikiano huo umewafanya kuweka mpango kazi na utekelezaji kutokomeza ujangili katika eneo hilo.
SOURCE: NIPASHE
30th December 2013

0 comments: