Friday, 27 December 2013

WAGANGA NA WAKUNGA WATIBA ASILIA TANZANIA WAKUBALI KUBEBA ZIGO LA MAUJI YA VIKONGWE

Uwawata yakubali kubeba zigo la mauaji ya vikongwe

Waganga wa jadi

Umoja wa Waganga na Wakunga wa Tiba Asilia Tanzania (Uwawata), umetangaza rasmi kubeba zigo la kushughulikia tatizo la uhalifu ikiwamo kukomesha mauaji ya kikatili kama vile ya albino na vikongwe nchini.

Aidha, umoja huo umewaagiza waganga na wakunga wa tiba asilia nchini, kujisajili kwenye umoja huo na kuacha kufanya shughuli zao kibiashara kwa kuwa kazi ya tiba ni huduma na siyo biashara.


Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa taifa wa Uwawata, Dk. Rashid Tengeza, kwenye mkutano mkuu wa mkoa uliofanyika mjini hapa juzi.


Tengeza alisema Uwawata ina jukumu la kuhakikisha matendo ya kikatili na kishirikina yanakoma na kuifanya jamii na taifa kuwa na amani.


Kwa mujibu wa Dk. Tengeza, ambaye pia aliongozana na Katibu Mkuu wa taifa wa umoja huo, Dk. Daud Nyaki, chanzo cha mitafaruku, uchochezi na mauaji, ni ramli chonganishi zinazopigwa na waganga wa tiba asilia wasio waaminifu.


“Sisi waganga wa tiba asili ndiyo wenye jukumu la kulipoza taifa hili na kuwa la amani kwani majanga yanayotokea ni waganga wa tiba asilia wasio waaminifu kujihusisha na matendo kama vile uchochezi, mitafaruku na mauaji,” alisisitiza Dk. Tengeza.


Alisema ufike wakati waganga kudhibitiana wenyewe kwa wenyewe na kwamba serikali inatarajia kuona matunda ya umoja huo ikiwa ni kukomesha mauaji ya vikongwe na albino ambayo hufanywa ama kuchochewa na waganga matapeli.


Naye Dk. Nyaki akizungumza kwenye mkutano huo aliwataka waganga kuacha kuchukua fedha za majambazi kwa madai ya kuwakinga wasikamatwe na polisi kwani kufanya hivyo ni kuhatarisha maisha yao na taifa kwa ujumla.


Aidha, alisema chini ya umoja huo, waganga wawe kiungo kati ya serikali na wananchi ambao ni wateja wao na kufichua kila uovu unaofanyika kwenye maeneo yao na kubainisha kuwa kila mganga atakayefanya hivyo, umoja huo utakuwa mtetezi wake anapopata matatizo.


Katika mkutano huo, uongozi wa Uwawata mkoa ulijaza nafasi za wajumbe zilizokuwa wazi ndani ya kamati ya utendaji.


Waliochaguliwa kuziba nafasi hizo ni Mwenyekiti wa Mkoa, Allan Nkong’ota, Makamu Mwenyekiti, Bakari Mwinjuma, Katibu wa Mkoa Omari Sinde na Zaina Mkama, msaidizi wake.


Hata hivyo, katika uchaguzi huo uliyosimamiwa na Dk. Nyaki, iliundwa pia kamati maalumu ya mkoa ya watu 10 na kupewa jukumu la kufichua uhalifu, kukomesha waganga matapeli, rambaramba, wapiga ramli chonganishi, mauaji ya albino na vikongwe.


Alisema kuwa kamati kama hiyo zimeundwa katika mikoa mbalimbali kwa lengo la kukabiliana na matendo maovu na mauaji ya vikongwe, albino na kushughulikia waganga matapeli wanaochonganisha jamii, kazi ambayo aliieleza kuwa inafanywa kwa ushirikiano baina ya kamati na polisi wa eneo husika.


Waliochaguliwa kwenye kamati hiyo ambayo ilishirikisha wataalam kutoka taasisi mbalimbali nje ya umoja huo, ni Mwenyekiti wa Kamati, Juma Lukuwa, (mganga) Katibu ni Dege Masoli (mwaandishi wa habari NIPASHE).


Mjumbe mwingine nje ya umoja huo ni mwandishi wa habari wa gazeti la Tanzania Daima, Elizabeth Kilindi na Abdallah Hamisi, Salehe Chamshama, Mayasa Jabu, Mwajuma Bakari, Mavumba Zuberi, Theresia Basilio na Kuruthumu Hossein. 
 
SOURCE: NIPASHE
27th December 2013

0 comments: