Thursday, 26 December 2013

WATOTO 150 WAZALIWA MKESHA WA KRISMASI NCHI NZIMA

 
Jumla ya watoto 150 wamezaliwa katika mkesha wa Sikukuu ya Krismas kwenye hospitali za mikoa mbalimbali nchini, kati yao wa kike wakiwa 56 na wa kiume 93.
DAR ES SALAAM
Kati ya watoto hao, 122 wamezaliwa katika Hospitali za Mwananyamala, Amana, Temeke na Muhimbili, jijini Dar es Salaam, wa kiume wakiwa ni 81 na wa kike 41.
Muuguzi wa zamu Hospitali ya Mwananyamala,Tuswege Mwamwaja, alisema watoto 42 walizaliwa katika hospitali hiyo, huku 16 wakiwa ni wa kike na 22 wa kiume.
Pia muuguzi wa zamu katika Hospitali ya Amana, Agnes Simon alisema watoto waliozaliwa katika hospitali hiyo ni 38, kati yao wa kiume ni 26 na wa kike ni 12.
Vilevile, Muuguzi wa zamu katika Hospitali ya Temeke, Happy Kimbawala, alisema kati ya watoto 36 waliozaliwa katika hospitali hiyo, wa kiume ni 24 na wa kike ni 12.
Muuguzi wa zamu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema kati ya watoto sita waliozaliwa katika hospitali hiyo, wote ni wa kiume.
RUVUMA
Mkoani Ruvuma, watoto 19 walizaliwa katika mkesha huo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo iliyopo mjini Songea, ambao kati yao, saba ni wa kiume na 12 ni wa kike.
Afisa Muuguzi Msaidizi wa Hospitali hiyo, Amina Mwambe, alithibitisha na kusema katika siku za kawaida huzaliwa watoto, kuanzia 25 hadi 30.
SINGIDA
Mkoani Singida, watoto tisa walizaliwa wakati wa mkesha katika Hospitali ya Mkoa wa Singida na Kituo cha Afya Sokoine cha Halmashauri ya Manispaa ya Singida Muuguzi wa zamu katika wodi ya wazazi ya Hospitali ya Mkoa wa Singida, Constansia Muna, alisema miongoni mwa watoto hao, watano ni wa kiume na  watatu ni wa kike.
Naye muuguzi wa zamu katika wodi ya wazazi ya kituo hicho, Teresia Nkui, alisema wakati wa mkesha wa Krismasi, alizaliwa mtoto mmoja wa kiume.
Kwa mujibu wa wauguzi wote, na afya za watoto na mama zao wote zinaendelea vizuri.
Imeandaliwa na Enles Mbegalo (Dar), Nathan Mtega (Songea) na Elisante John (Singida).
CHANZO: NIPASHE
26th December 2013

0 comments: