Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba
Kauli hiyo aliitoa jana mjini hapa katika mkutano wa kuchagua wawakilishi wa Asasi zisizo za kiserikali ili majina yao yapelekwe kwa Rais kwa ajili ya kuyateua kushiriki kwenye Bunge Maalum la Katiba linalotarajia kufanyika Februari mwakani.
Kibamba alisema mpango huo unaosukwa ili Bunge hilo lisionyeshwe moja kwa moja na vituo vya televisheni nchini hautakubalika na mambo yote yanatakiwa kuwa hadharani.
Alisema Bunge hilo lisiwe la kificho ili kila mwananchi ashuhudie kinachoendelea ndani ya Bunge hilo.
“Lazima tuone moja kwa moja…tuone wabunge wanaolala, wanaochapa kazi, wanaoleta vijembe nao waonekane…sisi Jukwaa la Katiba kila siku jioni tutakuwa kwenye makorido mnapotoka tunawasubiri ili tuwaambie walichokifanya,” alisema.
Pia, alisema kuna dharau ambazo zinaendelea bungeni na kuwa wabunge wapya wa kiingia wale wakongwe wamekuwa wakiwaita wale wapya kuwa ni wachanga.
“Kuna baadhi ya wabunge wakongwe ambao wana zaidi ya miaka 30 bungeni, wanapowaona wale wachanga wanazungumza wanawaambia nyie watoto ebu nyamazeni hamjui kitu hapa,” alisema.
Aidha, aliwataka Babunge na Wawakilishi kutowanyanyapaa wabunge watakaoteuliwa na Rais kwa ajili ya Bunge Maalum la Katiba.
Hata hivyo, alisema Jukwaa la Katiba litatumia nafasi hiyo kuwafunda na kutoa mwongozo kwa wawakilishi ambao watachaguliwa kuingia katika Bunge hilo ili kuhakikisha kuwa wanawatetea Watanzania.
Bunge hilo linatarajiwa kushirikisha wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 358, Wawakilishi wa Zanzibar 76 na Asasi wawakilishi 201.
Jana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein walikabidhiwa Rasimu ya pili ya Katiba na kinachosubiriwa ni majina ya wawakilishi kutoka asasi hizo na mwisho wa kutuma majina yao ni kesho kutwa.
Baada ya hapo Bunge hilo litakutana na kuipitisha katiba. Watakaofanya maamuzi ya mwisho ya kuikubali au kuipitisha katiba hiyo ni wananchi kupitia kura ya maoni.
SOURCE:
NIPASHE
31st December 2013
0 comments:
Post a Comment