Aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Marehemu ,Dk. Sengondo Mvungi
Washtakiwa 10 wanaotuhumiwa na mauaji ya Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk. Sengondo Mvungi, jana waliomba mahakama kuwatenganisha katika mahabusu tofauti kwa madai ya kutishiana kuuana wanapokaa gereza moja.
Ombi hilo liliwasilishwa jana na aliyekuwa mlinzi wa Dk. Mvungi ambaye ni mshtakiwa wa nne, Longishu Losingo (29), mbele ya Hakimu Mkazi Sundi Fimbo, anayesikiliza usikilizwaji wa awali wa kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Losingo alidai kuwa washtakiwa wanatishiana kuuana na wakati mwingine hugeuza mahabusu ukumbi wa masumbwi kwa kupigana ngumi na kusababisha uvunjifu wa amani.
“Mheshimiwa tunaomba ututenganishe kwa sababu tunatishiana kuuana huko mahabusu kutokana na kutajana wenyewe kwa wenyewe dhidi ya tuhuma hizi zinazotukabili… tunaomba mahakama itusaidie kututawanyisha,” alidai mshtakiwa huyo kauli ambayo iliungwa mkono na mshtakiwa mwingine.
Hakimu Fimbo alisema kwa bahati mbaya mahabusu iko moja na kwamba wanatakiwa kuelewana badala ya kusababisha uvunjifu wa amani wakati wakisubiri hatma ya kesi yao wataendelea kukaa katika mahabusu moja.
Kabla ya kuwasilishwa malalamiko hayo, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Yasinter Peter, ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Hakimu Fimbo alisema kesi hiyo itatajwa Desemba 19, mwaka huu na washtakiwa wataendelea kukaa mahabusu.
Mbali na Losingo, washtakiwa wengine ni wafanyabiashara Chibago Magozi maarufu kama Chiligati (32), mkazi wa Vingunguti, John Mayunga ama Ngosha (56), mkazi wa Kiwalani na Juma Kangungu (29), mkazi wa Vingunguti.
Wengine ni Masunga Msukuma (40), mkazi wa Kitunda, Paulo Mdonondo (30), mkazi wa Tabata Darajani na Mianda Mlewa ama White (40), mkazi wa Vingunguti Shule ya Tapa. Washtakiwa wengine ni Zacharia Msese (33), mkazi wa Buguruni Ghana kwa Hawa Masoud, Msigwa Matonya (30), mkazi wa Vingunguti Machinjioni na Ahmad Kitabu (30), mkazi wa Kinondoni Mwananyamala.
Ilidaiwa kuwa Novemba 3, mwaka huu, eneo la Msakuzi Kibwegere, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, washtakiwa kwa pamoja na kwa makusudi walimuua Dk. Mvungi.
Washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote hadi pale upelelezi wa kesi yao utakapokamilika na kesi hiyo itahamishiwa Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Dar es Salaam.
SOURCE:
NIPASHE
6th December 2013
0 comments:
Post a Comment