WATU wawili wamekufa na wengine watatu wamepoteza fahamu,wote wakiwa
ni wakazi wa kitongoji cha Chanji Soweto mjini Sumbawanga mkoani
Rukwa, baada ya kukosa hewa wakiwa ndani ya
shimo la kisima cha maji walilokuwa wakichimba.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda alisema kuwa tukio
hilo lilitokea jana nyakati za saa mbili asubuhi katika kitongoji
hicho na kuwataja waliofariki kuwa ni Juma Kaniki (43) na Jonas
Mwamburutu (37) ambao walikuwa wakifanya kibarua cha kuchima shimo la
maji nyumbani kwa Patrick Mwakyusa (37).
Katika tukio hilo awali mwenye nyumba hiyo alimwajiri Mwamburutu
kufanya kazi ya kusafisha kisima hicho ambacho kilichimbwa na kujengwa
miezi mitatu iliyopita lakini kilishindwa kutoa maji hali
iliyomlazimu kukifanyia usafi ili kiweze kutoa maji.
Licha ya Mwamburutu kukbali kufanya kazi hiyo lakini alipoingia
alishindwa kutoka na ndipo mwenye nyumba hiyo alipoomba msaada wa watu
ili kuweza kumtoa lakini watu watatu wa mwanzo walioingia kwa nyakati
tofauti waliishia njia na kuomba msaada wa kutolewa ndani ya shimo
hilo wakilalamikia kukosa pumzi.
"Baada ya watu hao kushindwa ndipo alipokuja huyo Juma , akasema yeye
anaweza kumtoa mtua aliyekuwamo ndani ya kisima hicho ndipo
tulimshauri kuwa tumfunge kamba kwanza ili akiishiwa pumzi tumvute
lakini alikataa akidai kuwa yeye ni mzoefu, na alifanikiwa kufika hadi
alipo marehemu na alimfunga kamba na kututaka tumvute, lakini kabla
hatujafanyahivyo alianza kupiga kelele kuwa naye anaishiwa pumzi,
baadaye akafa" alisema mmoja ya majirani ambaye hakutaka kutajwa jina
lake.
Harakati za kutoa miili ya marehemu hao ndani ya kisika hicho
kinachokadiriwa kuwa na urefu wa futi 24 ziliendelea kuanzia sa 5
asubuhi ambapo watu watatu tofauti wakiwapo askari polisi na wale wa
kikosi cha Zimamoto kwa kushirikiana na raia ziliendelea ambapo watu
wawili zaidi walioingia ndani kisima hicho walipoteza fahamu na
kukimbizwa hospitali.
"Jioni ya ilitulazimu kuanza kuchimba kisima hicho pembe kwa udongo na
ndipo alipofika mtu aliyejiita kuwa ni mganga wa jadi na liingia ndani
ya kisima baada ya kujipaka madawa lakini alizidiwa na kutolewa nje
akiwa na hali mbaya huku akipiga makelele ya kuomba msaada, huku
baadhi ya waokoaji wakizusha kuwa kulikuwa na kitu kilichodaiwa
kuwavuta wanapoingia ndani ya shimo hilo,". alisema mmoja wa waokoaji.
Juhudi za kuopoa miili ya marehemu hao zilifanikiwa saa mbili usiku
baada ya mtu mmoja aliyedai kuwa ni askari mstaafu wa JWTZ
aliyejitambulisha kwa jina moja la Kipatuka aliyezama mara tatu katika
shimo hilo na kufanikiwa kuwafunga kamba marehemu hao kisha miili ya
kuvutwa nje.
Akizungumza mara baada ya kukamilisha kazi ya kuopoa miili hiyo
Kipatuka alikanusha uwepo wa kitu kilichokuwa kikiwavuta marehemu hao
isipokuwa kulikuwa na mkandamizo mkubwa wa hali hewa kulikowafanya
marehemu hao kukosa pumzi na kuanguka kwa kutanguliza vichwa vyao
chini.
Hatahivyo licha ya tukio hilo umati mkubwa watu waliofika katika tukio
hilo walikosoa Idara ya Ardhi ya Manispaa ya Sumbawanga kuwaruhusu
watu wanaoishi kwenye eneo hilo kujenga karibu na mto Lwiche ambako
pia wamechimba visima vya maji ndani nyumba zao pasipo kibali, licha
ujenzi holela unaoendelea katika eneo hilo kiasi cha hata vyombo vya
uokoaji kushindwa kufika.
Na Elizabeth Ntambala, Sumbawanga
Mwisho.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment