Sunday, 29 December 2013

MPANGO WA BOMBA LA GESI LATOA AJIRA 400 NA WAZAWA WASIPUNGUA 200

Mradi wa ujenzi wa bomba la gesi umetengeneza ajira mpya 400 kwa vijana tangu ulipoanza Agosti.

Aidha, kuna mpango wa kuajiri wataalamu wa gesi, mafundi sanifu na mchundo wazawa wasiopungua 200 katika nafasi kadhaa kwenye mradi huo mapema mwakani.

Akizungumzia ajira hizo 400 Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Maliki Munisi alisema zilitolewa na wajenzi wasimamizi wa mradi huo ambao ni kampuni ya China ya CPDC kwa maelekezo ya TPDC.

"TPDC iliiagiza kampuni hiyo ifuate utaratibu wa kutoa kipaumbele cha ajira kwa wazawa katika maeneo yote ambayo 
Watanzania wana ujuzi nayo, ndipo waangalie utaratibu mwingine wa kugawa kazi hizo kwa wageni kama wazawa wanaoziweza hawatapatikana," Munisi alisema.

Kwa maelezo yake, ajira hizo ambazo hata hivyo si za kudumu kutokana na uhalisia wake ni pamoja na uchimbaji mitaro, usafishaji mkuza, usafirishaji mabomba kutoka eneo la hifadhi kwenda eneo la ujenzi, upakuaji na upakiaji mabomba kutoka bandarini na usuguaji mabomba kwa lengo la kuyasafisha baada ya kuyachomelea.

Kuhusu ajira za wataalamu na mafundi, Munisi alisema zitakuwa za kudumu tofauti na 400 zinazohusisha zaidi vibarua.

"Tunachosubiri ni kibali cha kuajiri kutoka Utumishi. Tayari tumekwishaandika barua inayoonesha mahitaji ya wataalamu wa gesi na mafundi 226 watakaotawanywa kwenye maeneo ya mradi. Kutokana na maendeleo mazuri ya mradi tunatarajia kuanza kutangaza ajira hizo mwakani kibali kitakapokuwa tayari," alisema na kuongeza kuwa utaratibu utakaozingatiwa ni kipaumbele kwa wazawa.

Mradi huo wa bomba lenye urefu wa kilometa 542 kutoka Mtwara na Songosongo mkoani Kilwa hadi Dar es Salaam unatarajiwa kukamilika kati ya Mei na Julai, mwakani. 

Hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi akifuatana na wadau wa maendeleo, alitembelea Kilwa kuangalia maendeleo ya mradi huo na kushuhudia mabomba ya urefu wa zaidi ya kilometa 142 yakiwa yameunganishwa.

Maswi alisema kuunganisha mabomba hayo kulianza Septemba hivyo kutokana na kasi ya ujenzi malengo ya serikali ya utandazaji yatakamilika kwa wakati uliopangwa.

Aliongeza kuwa, baada ya kukamilisha kazi hiyo, kitakachofuata ni kuchimba mtaro na kuyatandika hadi Julai mwakani kazi hiyo itakuwa imekamilika, na Desemba shehena ya kwanza ya gesi inatarajiwa kufika Dar es Salaam.

Ujenzi wa bomba hilo ulianza Agosti 15, na kupangwa kukamilika ndani ya miezi 18 kwa gharama ya Sh trilioni 1.9 ambazo ni mkopo kutoka benki ya Exim ya China. ---
 via Ziro99 blog

 

0 comments: