Na Goodluck Eliona, Mwananchi
Dar es Salaam. Serikali
imetangaza idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza
mwakani, huku 16,482 wakishindwa kuchaguliwa kutokana na uhaba wa
madarasa.
Wanafunzi hao ni kati ya 844,938 waliofanya
mtihani wa darasa la saba Septemba 11 na 12, 20013, ambapo 427,609
walifaulu kwa kupata alama A na C, ambayo ni sawa na asilimia 50.61 ya
ufaulu ikiwa ni ongezeko la asilimia 19 ikilinganishwa na matokeo ya
mwaka jana.
Akitangaza matokeo hayo jijini Dar es Salaam jana,
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (Tamisemi), Jumanne Sagini alisema jumla ya wanafunzi 867,983
walisajiliwa kufanya mtihani huo, lakini wanafunzi 23,045 hawakufanya
kutokana na utoro, vifo na ugonjwa.
Alisema kuwa kutokana na ongezeko la fursa ya
utoaji wa elimu ya sekondari nchini, wanafunzi 411,127 kati ya 427,609
waliofaulu mtihani wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika
shule za serikali awamu ya kwanza huku zaidi ya 16,000 wakikosa
kuchaguliwa kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa 412.
“Idadi hiyo ni sawa na asilimia 96.15 ya wanafunzi
waliofaulu mtihani. Kati ya wanafunzi hao wasichana ni 201,021 sawa na
asilimia 95.9 na wavulana ni 210,106 sawa na asilimia 96.3,” alisema
Sagini na kuongeza kuwa:
“Ninaziagiza Halmashauri zilizobaki katika awamu
ya kwanza ya uchaguzi kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa ili
kuwawezesha wanafunzi kujiunga na kidato cha kwanza ifikapo Machi 2013.”
Katibu Mkuu huyo aliongeza kuwa ikilinganishwa na
matokeo ya mwaka jana, idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kuingia kidato
cha kwanza imeongozeka kwa asilimia 31.37.
Alisema kuwa mtihani huo ambao ulifanyika Septemba
11 na 12, mwaka huu, ulisahihishwa kwa kutumia teknolojia ya kompyuta
‘Optical Mark Reader (OMR)’.
“Mwanafunzi aliyepata alama ya juu kabisa kwa
upande wa wavulana alipata 244 kati ya 250 huku msichana akipata 241.
Mwaka 2012 alama ya juu ilikuwa 237,” alisema.
Akizungumzia vitendo vya udanganyifu kwenye
mtihani huo, Sagini alibainisha kuwa wanafunzi 13 wamefutiwa matokeo
yao, ambayo ni idadi ndogo ikilinganishwa na watahiniwa 219 waliofutiwa
matokeo mwaka 2012.
“Napenda kutoa wito kwa walimu, wazazi na jamii
kwa ujumla kujiepusha na vitendo vya udanganyifu kwani vinatoa taswira
mbaya kwa taifa na kuwafanya watoto wetu wawe tegemezi zaidi kuliko
kujituma na kujibidiisha katika masomo,” alisema.
Hata hivyo, Katibu Mkuu huyo hakutaja viwango vya ufaulu kwa kila somo kama ambavyo imezoeleka katika mitihani iliyotangulia wala mkoa uliofanya vizuri au vibaya. Matokeo ya mwaka huu yanaonyesha kuwa idadi ya wanafunzi walioshindwa kufanya mtihani imepungua kwa wanafunzi zaidi ya 6,000 ikilinganishwa na 29,012 ambao hawakufanya mtihani huo mwaka jana.
0 comments:
Post a Comment