Friday, 27 December 2013

VIONGOZI WA SERIKALI WAOMBEWA MKOSA YAO NA MSAMAHA KWA MUNGU

Kiongozi wa kiroho, Nabii Cres1
Waumini wa huduma ya Mtakatifu Prince Mission yenye Makao Makuu yake Sinza jijini Dar es Salaam, wameomba msamaha wa Mungu kwa baadhi ya viongozi  wa umma kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni kuusaliti umma wanaoungoza.

Hatua hiyo inatokana na matumizi ya misahafu wanapokula viapo vya kuutumikia umma, kisha kutotimiza azma hiyo badala yake kujinufaisha binafsi na ‘kuwaangamiza’ raia wanaowachagua.


Kiongozi huyo wa kiroho, Nabii Cres1, aliwaambia waumini hao  wanaojulikana  kwa jina  la Wateule katika  ibada iliyofanyika mapema wiki hii kuwa, watu wengi  wamekuwa wakiapa bila  kujua  madhara yanatokana  na viapo hivyo.


“ Viapo vingine vinasababisha  mahangaiko  makubwa, na hii inatokana kukosa uaminifu binafsi, wapo wanaohangaika  kwa ajili ya hilo, tumuombe Mungu atuondolee adhabu hiyo,” alisema akiwalenga viongozi hao.


Alisema, baadhi  ya  viongozi  wa serikali duniani, wanaapa katika  maeneo mbalimbali kwa  kutumia vitabu vitakatifu ambavyo ni neno la Mungu, kuwa watenda kwa mujibu wa haki sawa na maslahi kwa watu wote, lakini wanapomaliza inakuwa kinyume chake.


“Baadhi yao  wanaapa  kuwa watalinda  mali za wananchi, watatenda haki, lakini badala  yake wanatenda tofauti na wengine wakijitajirisha wao na familia zao, jambo ambalo ni dhambi mbele za Mungu,”alisema.


Nabii Cres1, alisema miongoni mwa matendo yaliyo kinyume na viapo hivyo, ni kwa baadhi ya viongozi kuishi maisha ya kuhangaika moyoni na kukosa amani, kuondokewa na mvuto wa kupendwa na wananchi,  pamoja  na kuwa ana mali nyingi.


“Wengi unakuta wanaapa huku wakijua hawataweza kutenda kama  walivyoaapa. Inatakiwa kuwaombea msamaha kwa Mungu kwani viapo  visivyo vya dhati huleta madhara kwa jamii mzima,” alisema.


Aliongeza, “inakuwa laana kwa taifa, kama  tunapenda dunia ipone, lazima tuombee viongozi wote walioko madarakani, kuanzia ngazi ya juu hadi familia ili Mungu awawezeshe watende mema na kuzingatia viapo vyao kwa ustawi  wa taifa letu na jamii kwa ujumla.”

 
SOURCE: NIPASHE
28th December 2013

0 comments: