MKUU wa Mkoa (RC) wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma |
MKUU
wa Mkoa (RC) wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma, amewataka
wafanyabiashara mkoani hapa kuacha kupandisha bei ya vyakula katika
kipindi hiki cha Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya, na kwamba
watakaokiuka watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Dk. Ishengoma alitoa kauli hiyo alipokuwa akitoa salamu za Krismasi na kuwatakia heri ya Mwaka Mpya wakazi wa Mkoa wa Iringa.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini jana, mkuu huyo wa mkoa
aliwataka wakurugenzi wa halmashauri zote za wilaya kuanza kuzunguka
mitaani kuchunguza bei ya bidhaa na kuwachukulia hatua wote
wanaopandisha bei kiholela.
Alisema imekuwa ni kawaida kwa baadhi ya wafanyabiashara kutumia
sikukuu mbalimbali kujipatia fedha kwa kuwanyonya wananchi, jambo ambalo
katika mkoa huo halitavumiliwa.
Dk. Ishengoma alisema lengo la serikali ya mkoa kuwabana
wafanyabiashara ni kutaka kuona wananchi wanasherehekea sikukuu hizo
na kununua vyakula na vitu mbalimbali kulingana na bajeti
waliyoitenga.
Alieleza serikali ya mkoa haitakubali kuona wananchi wakiibiwa kwa
kuuziwa vyakula kwa bei kubwa na kuwaomba wananchi kutoa ushirikiano
katika suala hilo.
Pamoja na hayo, alivipongeza vyombo vya habari mkoani Iringa kwa
mchango mkubwa wa kuhamasisha maendeleo na kutaka kuonyesha
ushirikiano katika wakati huu wa sikukuu kwa kufanya uchunguzi wa
wafanyabiashara wanaopandisha bei.
0 comments:
Post a Comment