Zanzibar. Aliyekuwa Waziri wa
Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha amesema licha ya
kuvuliwa uwaziri ataendelea kuwa kiongozi wa kisiasa na kukitumikia
chama chake na wananchi bila ya kuvunjika moyo.
Nahodha, ambaye ni Mbunge wa Kuteuliwa ametoa kauli hiyo siku chache baada ya kuondolewa
kwenye Baraza la Mawaziri na Rais Jakaya Kikwete
kutokana na matatizo yaliyotokea katika utekelezaji wa Operesheni
Tokomeza Ujangili.
Akihutubia wanachama wa CCM waliomlaki na
kumsikiliza kwenye Ofisi ya chama hicho Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja
jana, Nahodha alisema yaliyomtokea ni mambo ya kawaida katika medani za
utumishi wa umma.
“Pamoja na hayo yaliyotokea, nitaendelea
kulitumikia taifa, chama changu na wananchi kwa uaminifu, juhudi na
uwezo wangu wote,” alisema Nahodha, ambaye pia ni Mwakilishi wa
Mwanakerekwe.
Alisema amewajibika serikalini kutokana na matakwa
ya wajibu katika utendaji wa pamoja na kusema kitendo hicho ni mfano wa
ajali inayoweza kumkuta mtu yeyote katika safari ya maisha.
“Sina kinyongo wala muhali, yaliyotokea ni mambo
ya kawaida katika medani za uongozi, wajibu na dhati yangu ni kuwa mtii
kwa Serikali zote. Pia kuitumikia CCM na kushirikiana na wananchi
wenzangu. Binadamu hawezi kujiepusha na mitihani, ”alisema Nahodha.
Alisema alikabidhiwa dhamana na viongozi wake ili kulitumikia taifa na kutimiza wajibu ipasavyo katika nyadhifa mbalimbali na yaliyomtokea ameyapokea kwa mikono miwili na hana kinyongo.
Mawaziri walioenguliwa pamoja na Nahodha ni Dk
Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani), Dk Mathayo David (Mifugo na Maendeleo
ya Uvuvi) na Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii).
Mapinduzi ya Zanzibar
Akizungumzia Mapinduzi ya Zanzibar, Nahodha alisema ni ufunguo uliofungua milango ya fursa kwa wananchi wanyonge waliokandamizwa na ukoloni huku akisifu uongozi kwa miaka minane wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, hayati Mzee Abeid Amani Karume.
Alisema kiongozi huyo licha ya kuongoza Mapinduzi
ya Januari 12, 1964, aliifanyia mema Zanzibar na watu wake katika
kuwaletea maendeleo na kwamba atakumbukwa na vizazi vyote hadi mwisho wa
dunia.
CHANZO Mwananchi gazeti
Ijumaa,Decemba27
2013
saa
8:45 AM
0 comments:
Post a Comment