Johannesburg. Kamati ya
Maandalizi ya Mazishi ya Kiongozi wa Wazalendo wa Afrika Kusini,Nelson
Mandela imeanza kupanga utaratibu wa mapokezi ya wageni mashuhuri
watakaohudhuria mazishi ya kiongozi huyo nchini Afrika Kusini.
Mandela alifariki nyumbani kwake kwenye Mji wa Houghton, Johannesburg, Alhamisi usiku. Alifariki akiwa na umri wa miaka 95.
Taarifa za jimbo zilizotolewa jana zilisema kuwa,
Uwanja wa Ndege wa Mthatha ulioko Eastern Cape utakuwa maalumu kwa
wageni mashuhuri zaidi watakaofika kwenye shughuli ya mazishi ya Nelson
Mandela.
“Watu hao mashuhuri zaidi, watapakizwa kwa pamoja
kwenye magari maalumu ya kifahari kupelekwa Qunu kuepuka vurugu katika
Barabara Kuu za N2,” alisema Noxolo Kiviet ambaye ni kiongozi wa jimbo
katika taarifa yake.
Watu mashuhuri wa kati na watu wa kawaida watatumia Uwanja wa Ndege wa Port Elizabeth na Uwanja wa Ndege wa East London.
Taarifa iliyotolewa jana ilieleza pia
kuwa,shughuli za kumuaga zitafanyika kwenye Uwanja wa FNB mjini
Johannesburg kesho kama ilivyopangwa na baadaye mwili wake kupelekwa
Qunu kwa taratibu nyingine kabla ya mazishi Jumapili ijayo.
Kiviet alisema,jimbo lake linajiandaa kupokea maelfu ya waombolezaji katika kipindi cha wiki moja.
“Shirika la Umeme,Eskom wametueleza kuwa
wamerekebisha upatikanaji wa umeme tangu Septemba na kuna mipango ya
dharura imewekwa endapo itatokea umeme kukatika.”
Alisema,benki, maduka na mashirika ya hisani yameongeza wafanyakazi na wamekuwa wakarimu kuwasaidia wale wote watakaokwama.
“Nimewaomba wananchi wa Eastern Cape kuwasaidia kuwapa malazi wageni wote watakaokwenda kwa maziko.”
Kiviet alisema, watu hawataruhusiwa kufika katika
baadhi ya maeneo na watatakiwa kuangalia katika maeneo yaliyotengwa
kuanzia Johannesburg hadi kwenye mazishi.
Mbali na hayo, baadhi ya maeneo yamekwishatengwa
kwa ajili ya kuaga ambayo ni; OR Tambo, Nelson Mandela Bay, Buffalo
City, Chris Hani, Queenstown, Joe Gqabi, Cacadu, Alfred Nzo na Wilaya ya
Amathole.
0 comments:
Post a Comment