Monday, 9 December 2013

UVCCM YAOMBA WILAYA YA RORYA WAPELEKEWE CHAKULA


Mkuu wa Mkoa Mara,John Tupa

Jumuiya  ya Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Wilaya ya Rorya mkoani Mara, imeiomba serikali kupeleka chakula cha msaada katika wilaya hiyo kutokana na mvua kuchelewa na kusababisha njaa kwa wananchi wake.

Ombi hilo lilitolewa mjini hapa jana na Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM Mkoa wa Mara, David Wembe, alipokuwa akisoma maazimio ya kikao cha Baraza Kuu la Wilaya kilichofanyika mjini Utegi.


Wembe alisema kutokana na kuchelewa kwa mvua, hali ya chakula ni mbaya kwa wananchi wa wilaya hiyo.


"Tunaiomba serikali iwaangalie kwa jicho la huruma wananchi wa Wilaya ya Rorya kutokana na hali hiyo," alisisitiza Wembe.


Mbali na hilo, kikao hicho pia kiliipongea Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Kamati ya Siasa ya wilaya iliyokutana chini ya Mkuu wa Mkoa MaraJohn Tupa, na kufanikiwa kusuluhisha mvutano uliokuwapo kati ya Mbunge wa Rorya, Lameck Airo (CCM) na Mkuu wa wilaya hiyo.


Hata hivyo, kwa upande wake, Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Rorya, Sango Kasera, alisema jumuiya yao haikubaliani na kitendo cha baadhi ya viongozi wa Chama kuendelea kuchochea mgogoro huo ambao tayari umeshamalizika.


"Katika hili, UVCCM tunawataka viongozi wa Chama ngazi ya wilaya kuwa na moyo wa uvumilivu kwani malumbano yaliyokuwapo kati ya Mbunge na DC, yamemalizika na kuendelea nalo jambo hili ni kutowatendea haki wananchi," alisema Sango.
SOURCE: NIPASHE
9th December 2013

0 comments: