JK AMPONGEZA TENGA, AMTAKA ASICHOKE KUTOA USHAURI!
PAMBANO TANZANITE, BASETSANA LAINGIZA MIL 5/-
SOMA ZAIDI:
Release No. 207
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Desemba 8, 2013
MECHI YA KILIMANJARO STARS KUPIGWA MACHAKOS
Mechi ya kwanza ya nusu fainali ya
michuano ya mwaka huu ya Kombe la Chalenji kati ya Tanzania Bara
(Kilimanjaro Stars) na wenyeji Kenya (Harambee Stars) itapigwa Uwanja wa
Machakos.
Kwa mujibu wa ofisa wa CECAFA, Amir
Hassan mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Machakos ulioko takribani kilometa
64 kutoka jijini Nairobi. Mechi hiyo itachezwa Jumanne (Desemba 10
mwaka huu) kuanzia saa 10 kamili jioni na itaoneshwa moja kwa moja na
kituo cha televisheni cha SuperSport kupitia chaneli ya SS9.
Kilimanjaro Stars imetinga hatua hiyo
baada ya kuivua ubingwa Uganda (The Cranes) kwa mikwaju 3-2 ya penalti
katika mechi ya robo fainali ya michuano hiyo iliyochezwa jana Uwanja wa
Aga Khan katika Jiji la Mombasa.
Hadi dakika 90 za kawaida zinamalizika
timu hizo zilikuwa zimefungana mabao 2-2. Mabao ya Kilimanjaro Stars
yalifungwa na Mrisho Ngasa wakati katika mikwaju ya penalti walofumania
nyavu ni Amri Kiemba, Athuman Idd na nahodha Kelvin Yondani.
JK ATOA CHANGAMOTO KWA UONGOZI MPYA TFF
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ametoa
changamoto kwa uongozi mpya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) kusukuma mbele zaidi gurudumu la maendeleo ya mchezo huo nchini.
Ametoa changamoto hiyo katika barua yake
kwa Rais mstaafu wa TFF, Leodegar Tenga na kumtaka asichoke kutoa
ushauri na uzoefu wake kila utakapohitajika katika shughuli mbalimbali
zinazohusu maendeleo ya mpira wa miguu Tanzania.
Rais Kikwete ametoa changamoto hiyo
wakati akijibu barua ya Tenga iliyokuwa ikimuarifu kuhusu kumaliza
kipindi chao cha uongozi, na kumshukuru yeye binafsi (Rais Kikwete) na
Serikali anayoiongoza kwa mchango waliotoa katika kuendeleza mpira wa
miguu nchini.
“Pongezi zako zimetupa moyo na ari ya
kuongeza maradufu juhudi zetu za kuboresha kiwango cha ubora wa mchezo
wa mpira wa miguu nchini.
“Kwa niaba ya Serikali napenda kuchukua
nafasi hii kutoa pongezi za dhati kwako wewe na uongozi wote uliopita wa
TFF kwa mchango wenu muhimu mlioutoa wa kuendeleza mpira wa miguu
nchini.
“Mafanikio ya kutia moyo yamepatikana
chini ya uongozi wako,” amesema Rais Kikwete katika barua yake hiyo na
kumtakia kila la heri Tenga katika shughuli zake.
Hata hivyo, ameongeza kuwa Tanzania bado
haijafika pale ambapo inapataka, lakini dalili njema zimeanza
kuonekana, hivyo kinachotakiwa sasa ni uongozi mpya kusukuma mbele zaidi
gurudumu la kuendeleza mpira wa miguu nchini.
Tenga ambaye hivi sasa ni mjumbe wa
Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na
Kati (CECAFA) aliiongoza TFF kwa vipindi viwili kuanzia Desemba 2004
hadi Oktoba 2013.
PAMBANO LA TANZANITE LAINGIZA MIL 5/-
Pambano kati ya timu ya Taifa ya
wanawake kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 ya Tanzania (The
Tanzanite) dhidi ya Afrika Kusini (Basetsana) lililochezwa jana (Desemba
7 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam limeingiza sh. 5,353,000.
Washabiki waliohudhuria mechi hiyo ya
kwanza ya raundi ya pili ya Kombe la Dunia, Kanda ya Afrika
iliyomalizika kwa The Tanzanite kulala mabao 4-1 walikuwa 4,282.
Viingilio vilikuwa sh. 1,000, sh. 2,000, sh. 5,000 na sh. 10,000.
Mgawo wa mapato hayo ulikuwa kama
ifuatavyo; Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 816,559.32, gharama za
kuchapa tiketi sh. 1,649,754, asilimia 20 ya gharama za mchezo sh.
577,573) wakati wamiliki wa uwanja walipata sh. 433,003.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika
(CAF) lilipata sh. 144,334.33 huku Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) likipata sh. 1,732,012.01.
Mechi iliyopita ya Tanzanite dhidi ya
Msumbiji iliyochezwa Oktoba 26 mwaka huu Uwanja wa Taifa, na timu hiyo
kushinda mabao 10-0 ilishuhudiwa na watazamaji 5,003 na kuingiza sh.
6,190,000.
Tanzanite na Basetsana zitarudiana kati ya Desemba 20 na 22 mwaka huu jijini Johannesburg, Afrika Kusini.
Boniface Wambura Mgoyo
Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 comments:
Post a Comment