ASEMA WATANZANIA ZAIDI YA 500 WASHIKILIWA NCHI ZA NJE,WENGINE 100 WASUBIRI KUNYONGWA NCHINI CHINA
KATIBU
Mkuu wa wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na watoto Anna Maembe
ametaka vijana vijana nchini kuachana kabisa na biashara ya dawa za
kulevya kwani inawasababishia matatizo makubwa katika maisha yao badala
yake wajiunge na kutengeneza vikundi vya kijasiriamali ili serikali
iweze kuwasaidia kujikwamua kimaisha na kufikia ndoto zao.
Amesema
takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa, zaidi ya vijana 500 wa
Kitanzania wako kizuizini katika nchini tofauti duniani walikokamatwa
wakisafirisha dawa hizo, huku vijana wengine wapatao 100 wakiwa
wamehukumiwa kunyongwa nchini China.
Aliyasema
hayo alipokuwa akizungumza na makundi mbalimbali ya kijamii wakati wa
ziara yake katika kata ya Matai wilayani Kalambo Mkoa wa Rukwa jana,
ambapo alisema biashara hiyo inachafua sana jina la Tanzania katika
Jumuia ya Kimataifa kutokana na idadi kubwa ya vijana kujihusisha na
biashara hiyo.
Akizungumzia
sera ya Jinsia inayotekelezwa na wizara yake, Katibu Mkuu huyo alisema
haina lengo la kuwafanya wanawake kuwatunishia misuli wanaume katika
familia bali ni kuwawezesha wanawake kushiriki katika uzalisha na kukuza
kipato cha familia na taifa kwa ujumla ili kukabiliana na gharama za
maisha ambazo zimepanda sana kwa sasa.
Vilevile
alitoa wito kwa wazazi kuhakikisha wanatenga muda wa kukaa na
kuzungumza na watoto ili kujua changamoto zinazowakabili ikiwemo
unyanyasaji wa kijinsi na kisaikolojia wanazokumbana nazo na pia
kuwapatia haki zao za kimsingi kama elimu, afya na kusikilizwa kama
ambavyo sera ya watoto hapa nchini inavyoelekeza.
Katika
kuimarisha vikundi vya wanawake mkoani Rukwa, katibu mkuu Maembe ametoa
shilingi milioni 43 kutoka katika wizara yake, ambapo vikundi kutoka
katika Halmashauri za wilaya ya Nkasi, Kalambo, Sumbawanga Vijijini na
Manispaa vitanufaika kwa mtindo wa wanachama wa vikundi hivyo kupatiwa
mikopo kwa ajili ya kutekeleza shughuli zao za kiuchumi.
NA RAMADHANI JUMA,
AFISA HABARI OFISI YA MKURUGENZI-KALAMBO
0 comments:
Post a Comment