KAMPENI za uchaguzi mdogo wa ubunge
jimbo la Kalenga wilayani Iringa zimeingia katika sura mpya baada ya Chama cha
Mapinduzi (CCM) kudai kuwepo kwa njama kutoka kwa wapinzani wao za kuwateka
nyara baadhi ya viongozi wake.
Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa,
Hassana Mtenga aliyasema hayo kwenye kampeni za kumnadi mgombea wao Godfrey
Mgimwa zilifanyika juzi katika kijiji cha Mseke.
Mtenga alisema “Taarifa za uhakika
kutoka ndani ya moja ya vikao vyao vya wafuasi wa Chadema vilivyofanyika
hivikaribuni mjini Iringa, kulikuwepo na hoja ya yeye na Mwenyekiti wa CCM Mkoa
wa Iringa, Jesca Msambatavangu kutekwa ili kudhohofisha kampeni,” alisema.
Alisema taarifa za uhakika walizopata
kutoka kwa wafuasi wao walioko ndani ya chama hicho zinaonesha kuwepo na kundi
la vijana zaidi ya 50 kutoka mikoa mbalimbali nchini waliokuja wilayani Iringa
kwa kazi maalumu.
Akiwahusisha vijana hao na baadhi ya
matukio ya uhalifu, Mtenga aliwataja majina na namba zao za simu huku akiwaomba
Polisi kulifanyia kazi suala hilo.
Hata hivyo alisema CCM imejipanga kikamilifu
kukabiliana na vurugu zozote watakazofanyiwa na wapinzani wao hao.
“Ikitoke mfuasi wetu au mwanachama wetu
amefanyiwa chochote kile na kundi hilo la Chadema, nawaambia huo ndio unaweza
kuwa mwisho wa kampeni za Chadema katika jimbo hili,” alisema.
Alisema mwanaCCM au mwananchi yoyote
atakayefanyiwa fujo na wafuasi hao wa Chadema atoe taaarifa kwa viongozi wa
kata ili hatua dhidi yao ziweze kuchukuliwa mara moja.
Akizungumzia vuguvugu la mabadiliko
maarufu kama M4Cs, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa alisema mabadiliko hayo
yanalenga kuwatoa watanzania kutoka kwenye amani kwenda kwenye machafuko.
Alisema machafuko yakakapoanza, watakaopata
madhara ya haraka ni watanzania wa kawaida kwasababu familia za wanaoyahamasisha hazitakuwepo.
“Pale Iringa Mjini tuna mbunge wa
upinzani, muulizeni kama watoto wake huwa anawatanguliza kwenye maandamano
wanayoitisha mara kwa mara; haijawahi kutokea na haitatokea, mtakaotangulizwa
mbele ni nyie,” alisema.
Akitoa mfano wa vurugu zilizotokea
wilayani Kilolo wakati wa uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya Ukumbi, alisema
vijana watatu waliokuwa wafuasi wa Chadema walikamatwa na baada ya kukamatwa
hawakupata msaada wowote kutoka kwa viongozi wa chama hicho.
“Tulikamatwa katika vurugu tulizopanga
kuzifanya katika ya Ukumbi, lakini hatukupata msaada baada ya kufikishwa
Polisi; aliyetusaidia chai na chakula tukiwa mahabusu ni huyu huyu Mwenyekiti
wa CCM Mkoa,” alisema mmoja wao Filbert Kisumbo.
Kisumbo alisema baada ya kuachiwa, hakuna
kiongozi wa Chadema aliyekuwa tayari kuwasaidia nauli ya kurudi makwao na ndipo
walipoenda kumuangukia Mwenyekiti wa CCM kwa mara nyingine tena ili wasaidiwe.
“Hatukuwa na neno la ziada la shukrani zaidi ya kumwambia hatuna sababu ya kuendelea kuwa wana Chadema; kama kwenye shida kila mmoja na lwake na kwenye raha wanaofaidi ni wakubwa, tukaona ni bora tujiunge CCM,” alisema na kuwataja wenzake kuwa ni Steven Mkimbo na Daudi Mwenda.
0 comments:
Post a Comment