Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen
wamekubaliana kuvunja mkataba katika makubaliano ambayo ni siri kwa
pande zote mbili.
Uamuzi
huo umetangazwa leo (Februari 27 mwaka huu) jijini Dar es Salaam kwa
pamoja na Rais wa TFF, Jamal Malinzi na Kocha Poulsen mbele ya waandishi
wa habari.
Rais
Malinzi kwa niaba ya TFF ametoa shukrani za dhati kwa Kocha Poulsen kwa
ushirikiano na mchango ambao ameutoa kwa Tanzania kuanzia kwenye mpira
wa miguu wa vijana.
Naye Kim
amewashukuru Watanzania kwa ushirikiano waliompatia kwa kipindi cha
miaka mitatu alichokaa nchini kuanzia Mei 2011 alipoteuliwa kuwa kocha
wa timu za Taifa za vijana, na baadaye Taifa Stars.
Akizungumzia
benchi jipya la ufundi la Taifa Stars, Rais Malinzi amesema
linatarajiwa kutangazwa hivi karibuni likiongozwa na kocha kutoka nje ya
Tanzania.
Amesema
kwa upande wa mechi dhidi ya Namibia itakayochezwa Machi 5 mwaka huu
jijini Windhoek, Stars itaongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Ufundi, Salum
Madadi akisaidiwa na kocha Hafidh Badru kutoka Zanzibar.
Katika
hatua nyingine, Kocha Madadi amewaondoa wachezaji watano wa Yanga katika
kikosi kilichotajwa awali ili wapate fursa ya kuitumikia timu yao
kwenye mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al-Ahly ya Misri.
Wachezaji
hao ni Athuman Idd, David Luhende, Deogratius Munishi, Frank Domayo,
Kelvin Yondani na Mrisho Ngasa. Pia kipa Ivo Mapunda ameondolewa katika
kikosi hicho baada ya kupata msiba.
Nafasi
zao zimezibwa na wachezaji Abdi Banda (Coastal Union), Himid Mao (Azam),
Juma Luizio (Mtibwa Sugar), Said Moradi (Azam) na Shabani Kado (Coastal
Union).
Taifa
Stars itaingia kambini keshokutwa (Machi 1 mwaka huu) jioni kwenye
hoteli ya Accomondia jijini Dar es Salaam, na itaondoka Machi 3 mwaka
huu alfajiri kwa ndege ya South African Airways na kurejea nchini Machi 7
mwaka huu saa 8.15 mchana.
TWIGA STARS IMEWIVA, SHEPOLOPOLO YATUA
Wakati
Zambia (Shepolopolo) imewasili leo mchana (Februari 27 mwaka huu), Twiga
Stars imesema mazoezi yamewaingia barabara tayari kwa mechi dhidi ya
Wazambia hao itakayochezwa kesho (Februari 28 mwaka huu).
Mechi
hiyo ya marudiano ya raundi ya kwanza ya michuano ya Afrika kwa Wanawake
(AWC) itafanyika Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi kuanzia saa 10
kamili jioni, na hakutakuwa na kiingilio.
Wakizungumzia
mechi hiyo, Kocha wa Twiga Stars, Rogasian Kaijage na nahodha wa timu
hiyo Sophia Mwasikili wamesema kikosi chao kimewiva kwa ajili ya
mpambano huo baada ya kufanyia kazi upungufu uliojitokeza katika mechi
ya kwanza.
Twiga
Stars ilipoteza mechi ya kwanza iliyochezwa Februari 14 mwaka huu jijini
Lusaka kwa mabao 2-1, na inahitaji ushindi ili iweze kusonga mbele
kwenye michuano hiyo ambayo fainali zake zitafanyika Oktoba mwaka huu
nchini Namibia.
Iwapo
Twiga Stars itafanikiwa kuitoa Zambia katika mechi hiyo itakayooneshwa
moja kwa moja na Azam Tv itacheza raundi ya mwisho na Zimbabwe.
Msafara
wa Shepolopolo una watu 26 ambapo wachezaji ni Anita Mulenga, Annie
Kibanji, Carol Howes, Debora Chisanga, Emelda Musonda, Esther Mukwasa,
Grace Zulu, Hazel Nali, Hellen Mubanga, Lweendo Chisamu, Meya Banda,
Mirriam Katamanda, Misozi Zulu, Mupopo Kabange, Noria Sosala, Rachel
Lungu na Susan Banda.
Viongozi
ni Maclean Daka, Charles Bwale, Kaluba Kangwa, Enala Phiri, Cornelia
Chazura, James Nyimbili, Besa Chibwe, Dorothy Sampa na Kabungo Katongo.
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari na Mawasiliano
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 comments:
Post a Comment