Wednesday, 26 February 2014

SUGU:NIMEITULIZA MBEYA

sugu_ea66c.png  

    Mbeya. Jimbo la Uchaguzi Mbeya Mjini linafahamika kwa rekodi yake ya kipekee.
    Kwa muda mrefu lina rekodi ya kubadili wabunge kila baada ya miaka mitano. Hiyo imetokea kwa wabunge kama Polisya Mwaiseje (NCCR- Mageuzi), Benson Mpesya (CCM), miongoni mwa wengi.
    Kwa sasa linashikiliwa na Joseph Mbilinyi 'Mr ll' au Sugu kutoka Chama cha Maendeleo na Demokrasia (Chadema )
    .
    Mr ll au Sugu ambaye kiumri ana miaka 42 aliupata ubunge huo kwa mara ya kwanza katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 2010.
    Mbunge huyo ambaye pia ni msanii anaeleza mbinu alizofanya kulipata jimbo hilo, alichoahidi wakati wa uchaguzi, alivyotekelekeza na vikwazo anavyopata akiwa mbunge wa Mbeya Mjini, halmashauri ambayo inaongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
    "Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2010, Chadema kupitia mimi katika Jimbo la Mbeya tuliahidi kurudisha madaraka kwa wananchi.
    Uhuru wa biashara
    Tulitaka wananchi wawe na uhuru wa kufanya biashara bila bughudha, vijana wafanye kazi kwa uhuru na mama lishe waheshimiwe,'' anasema Sugu jina ambalo amelipata kutokana na sanaa ya muziki wa kufokafoka.
    Mbunge huyo anasema alilazimika kutoa ahadi hiyo kwa sababu wananchi kipindi hicho walikuwa wakikamatwa ovyo na polisi au mgambo na kusingiziwa kesi za uongo.
    Anasema vijana wanaofanya biashara ndogondogo na mamalishe mitaani na wale wanaouza matunda walikuwa wakisumbuliwa na askari wa jiji na kwamba kipindi hicho wakazi wa Mbeya walikuwa na maisha ya wasiwasi.
    ''Hivyo mimi niliingia na hoja ya kuwatetea wanyonge, wakiwamo waosha magari, Wamachinga na wenye bajaj ambao walikuwa wakizuiwa wasiendeshe vyombo vyao mitaa ya mjini na Barabara Kuu ya Dar es Salaam – Zambia,'' anasema.
    Katika kutekeleza hilo, Mr ll anasema baada ya kupata ubunge, amesimama kidete kuwatetea wafanyabiashara, mamalishe na wauzaji matunda katika mitaa mbalimbali ili mradi hawavunji sheria za usafi wa mazingira
    Sugu anasema pia aliwaahidi wananchi wa Mbeya kwamba akiwa mbunge atatetea kujengwa barabara za kisasa zinazoonyesha kwamba Mbeya ni jiji kweli na kwamba zisipopatikana atapigania Mbeya irudi kwenye manispaa ili kupunguza kero.
    Anasema aliwaahidi wakazi wa Mbeya kwamba katika kipindi chake watamwita ''Bwana barabara'' kwa sababu barabara za mitaa, vitongozji na jiji zitaboreshwa.
    Katika kutekeleza ahadi hiyo, Sugu anasema kitendo cha yeye kuwa mbunge kimechangia kwa kiasi kikubwa kutekelezwa kwa umakini wa ujenzi wa barabara kupitia mradi uliofadhiliwa na Benki ya Dunia.
    Anasema barabara za lami zenye urafu wa karibu kilometa 30 zimejengwa kwenye maeneo mbalimbali ya Jiji la Mbeya wakati nazo barabara za mitaa, vitongoji vingi zimeboreshwa.
    Pia, anasema mwaka 2010 aliahidi kupambana na rushwa kwa udi na uvumba kuboresha utendaji wa sekta za afya, ulinzi, elimu, umeme, na jiji lenyewe.
    Katika kutekeleza hilo anasema alianza kazi kwenye Hospitali ya Rufaa Mbeya ambako baadhi ya wafanyakazi walikithiri kwa rushwa.
    Anasema alishirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) kuwakamata baadhi ya wafanyakazi wapenda rushwa kwenye hospitali hiyo.
    Pia, anasema ametetea hospitali hiyo ipate magari ya kubeba wagonjwa, tayari gari limefika na lingine linakuja.
    Anaongeza kuwa amekuwa akifuatilia kwa karibu polisi wapenda rushwa na hata wafanyakazi wa mahakama, Tanesco, na jiji anapopata malalamiko kutoka kwa wananchi wa Mbeya.
    ''Niliahidi kushirikiana na wananchi kuwasaidia wajane na watoto yatima, na nimewasaidia wajane kwa kuweka mazingira mazuri ya wao kuendelea kufanya biashara bila bughudha,'' anaeleza.
    Hata hivyo, kwa upande wa yatima anasema amewasaidia kupitia Mfuko wa elimu aliouanzisha ambao unawasomesha watoto 200 katika shule mbalimbali za msingi na sekondari.
    Watoto hao wanapata msaada wa sare za shule, wengine wanalipiwa ada na kupewa vifaa vya shule.
    Pia, anashauri watoto yatima katika shule mbalimbai za Serikali wanaosoma kwa misaada wasamehewe michango mbalimbali ikiwamo ya ulinzi.
    Mwakilishi huyo wa wapigakura wa Mbeya anasema pia kwamba aliahidi kujenga mabwawa ya samaki katika kila kata ili kuongeza vipato vya wananchi, lakini suala hilo limekwama kutokana na migogoro ya kisiasa.
    Anaongeza kuwa katika kampeni zake za ubunge aliahidi kuizindua michezo kwa kuhakikisha wakazi wa Jiji la Mbeya wanapata burudani.
    Anasema 'mizuka imezinduka' na aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya Jumaa Idd aliamua kuinunua timu mkoani Arusha na kuipa jina la Mbeya City.
    ''Nasisitiza timu ni ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya, siyo ya Sugu, Chadema wala CCM , lakini ukiona vinaelea ujue vimeundwa,'' anasema na kuongeza kuwa wananchi wa Mbeya ndiyo wamiliki wa timu.
    Kuhusu wasanii anasema hajawapatia fedha, lakini amewasaidia katika kupigania haki za stika na kuzishauri redio zilizopo jijini Mbeya zipende kutumia nyimbo za wasanii wa Mbeya ili kuwatangaza.
    Changamoto
    Changamoto anazopata akiwa Mbunge wa Chadema kwenye Serikali ya CCM, Sugu anasema siasa siyo mchezo mchafu kama wahusika wote wanakuwa na nia moja ya kuongeza kasi ya maendeleo.
    Hata hivyo anasema wapo wanasiasa wachache wanaoichafua siasa kwa kukwamisha miradi ya maendeleo ya wananchi kutokana na kwamba miradi hiyo inasimamiwa na upinzani.
    Anaeleza kuwa Chadema ilibuni mradi wa kuhamasisha wananchi wa Jiji la Mbeya wawe na mabwawa ya samaki jambo ambalo pia linasisitizwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, lakini madiwani wa CCM wamemkwamisha.
    Anatoa mfano kwamba Kata ya Nsalaga ilichimba bwawa ambalo lingekuwa na samaki wenye thamani ya Sh14 milioni kila baada ya miezi mitatu, lakini madiwani wa CCM wamekwamisha.
    Pia, anasema Serikali iliyopo madarakani haipendi kutekeleza miradi ya manufaa kwa wananchi na taifa kwenye majimbo ya upinzani.
    Anatoa mfano wa Serikali kutojali kufufua viwanda vya nyama, mbolea, maziwa, sabuni, pembejeo vilivyokuwapo Mbeya.
    Anashauri tabia hiyo ikome, la sivyo itaondolewa kwa nguvu za umma.
    Anasema kwamba uchaguzi wa mwakani, 2015 ana uhakika kuchukua jimbo hilo tena na hatimaye madiwani wote kuwa wa Chadema na kuiongaza halmashauri ya jiji na kwamba hapo kasiya maendeleo ndipo itakapoonekana wazi.
    Hadi sasa Jimbo la Mbeya lina kata 36 ambapo Chadema inashikilia kata 17 kati ya hizo

    0 comments: