Monday, 24 February 2014

ALIYEMRUSHIA SARAFU ROONEY ADAKWA

wayne_rooney_akimwonesha_refa_sarafu_0f066.jpg
Mshambuliaji wa Manchester United, Wayne Rooney akimwonesha mwamuzi sarafu aliyorushiwa na mashabiki wa Crystal Palace wakati akienda kupiga kona timu hizo zilipopambana Jumamosi, juma lililopita.  Picha kwa hisani ya Action Images.
Na Fadhy Mtanga
MAMLAKA za kiusalama nchini Uingereza zinamshikilia shabiki mmoja wa Crystal Palace zikimtuhumu kurusha sarafu na kipande cha chupa kwa mshambuliaji wa Manchester United, Wayne Rooney, timu yake ilipokuwa mgeni wa Crystal Palace wikendi iliyopita.  Timu hizo zinazoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza zilikwaana katika dimba la Selhurst Park huku Mashetani Wekundu wakiibuka na ushindi wa magoli 2-0 yaliyotiwa kimiani na washambuliaji mahiri Robin van Persie aliyefunga kwa mkwaju wa penati na Wayne Rooney aliyeachia shuti kabambe.

Wakati Wayne Rooney akielekea kupiga mpira wa kona, shabiki mmoja alirusha sarafu huku mwingine akirusha kipande cha chupa kuelekea kwa mshambuliaji huyo. Mashabiki hao walikuwa katika jukwaa la Holmesdale. Wayne aliiokota sarafu hiyo na kuikabidhi kwa mwamuzi wa mchezo huo, Michael Oliver.
Baada ya mchezo huo, mamlaka ya soka nchini Uingereza (FA) iliagiza uchunguzi wa kina ufanyike ili hatua kali zichukuliwe kwa atakayepatikana na hatia ya kitendo hicho kinachotia doa mchezo huo unaopendwa zaidi ulimwenguni.  FA iliagiza kupitiwa kwa umakini kwa kamera za uwanjani, ripoti ya refarii pamoja na ripoti za maafisa usalama uwanjani hapo.  Tayari FA imesema yeyote atakeyapatikana na hatia hiyo atafungiwa kuingia uwanjani kutazama kabumbu.
Maafisa wa Met Police jijini London wamesema tayari shabiki huyo aliyedakwa amefikishwa katika kituo cha polisi cha South London.  Shabiki huyo anaendelea kuhojiwa.  Pia, uchunguzi zaidi unaendelea.
Hata hivyo, Wayne Rooney hakubughudhiwa na kitendo hicho kwani alihakikisha anafunga goli lake la kwanza ikiwa ni masaa 24 tu baada ya kusaini mkataba mpya.  Katika mkataba huo mpya utakaomweka klabuni hapo hadi 2019, mpachika mabao huyo mahiri wa Man United na timu ya taifa ya Uingereza atajikusanyia kitita cha paundi laki tatu kila wiki, kinachomfanya kuwa mchezaji aghali zaidi katika ligi ya kabumbu ya Uingereza.

0 comments: