Friday, 28 February 2014

UMOJA WA MATAIFA WAZINDUA KUMBUKUMBU ZA MAUWAJI YA RWANDA


tutu_cf5cb.jpg
Mmoja wa manusura wa mauaji ya maangamizi ya Rwanda ya mwaka 1994 akíwaombea wahanga wa mauaji mbele ya mafuvu yao katika kaburi la pamoja la Nyamata.
Umoja wa Mataifa umewasha mwenge kuzindua mkururo wa matukio yaliyopangwa kufanyika kwa nia ya kukumbuka miaka 20 ya mauaji ya maangamizi ya mwaka 1994 nchini Rwanda ambapo zaidi ya watu 800,000 waliuawa.
Akizungumza jijini New York katika kile kilichopewa jina la "Kwibuka 20", Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, alisema miaka 20 baada ya mauaji hayo ya maangamizi, kushindwa kwa jumuiya ya kimataifa kuzuia maafa nchini Syria ni jambo la aibu. Idadi ya washaopoteza maisha hadi sasa nchini Syria ni 140,000 kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.
Hata hivyo, Ban Ki-moon ameusifu uwezo wa Rwanda kuungana na kupatanisha baada ya mkasa huo na kusema umekuwa kivutio. Mauaji ya Rwanda yalianza masaa machache baada ya ndege iliyokuwa imembeba Rais Juvenal Habyarimana kuangushwa wakati ikikaribia mji mkuu, Kigali, tarehe 6 Aprili 1994.
Ndani ya siku 100 baada ya hapo, mauaji dhidi ya jamii ya Kitusti na Wahutu wenye msimamo wa wastani yaliangamiza roho za watu wapatao laki nane.
Wakati huo Umoja wa Mataifa ulikuwa na kikosi kidogo cha walinda amani nchini Rwanda, lakini Baraza la Usalama lilikataa kuongeza askari zaidi kukabiliana na mauaji hayo ya maangamizi, na hata nchi moja moja hazikutoa msaada wowote.
Syria kama Rwanda?
Hali inaonekana kufanana na hiyo kwa mauaji ya Syria, ambako hadi sasa bado Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limegawika vibaya juu ya mgogoro huo, ingawa Jumamosi iliyopita lilikubaliana kwa kauli moja juu ya azimio linaloyaruhusu mashirika ya misaada kuingia kwenye maeneo mbalimbali nchini humo.
Katika halfa hiyo ya hapo jana, Ban Ki-moon alisema licha ya Umoja huo kujifunza namna ya kuzuia maafa kama ya Rwanda, lakini hakuna uhakika kwamba matukio kama hayo hayawezi kujirejea.
"Mauaji ya maangamizi nchini Rwanda yalikuwa ni ishara kubwa ya kushindwa kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua dhidi ya uhalifu mbaya kabisa. Tunajua vyema zaidi sasa kuliko hapo kabla kwamba mauaji ya maangamizi si tukio moja tu, bali mchakato unaojumuisha mambo kadhaa na muda mrefu." Alisema Ban Ki-moon.
Ulaya nako kwatajwa
Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alizungumzia pia kupanda kwa kiwango cha chuki dhidi ya wahamiaji, Waislamu na jamii ya Waroma barani Ulaya na pia uvunjwaji mbaya kabisa wa haki za binaadamu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Umoja wa Mataifa unajaribu sasa kukabiliana na mauaji yanayochochewa kidini kwenye Jamhuri hiyo ya Afrika ya Kati, lakini hali inatajwa kuwa mbaya.
Wiki iliyopita, Ban Ki-moon alitoa wito wa kutumwa haraka kwa wanajeshi na polisi 3,000 ili kusaidiana na walinda amani 6,000 kutoka Umoja wa Afrika. Tayari wanajeshi 1,6000 wa Ufaransa wako huko, na Umoja wa Ulaya umeahidi kutuma wengine 500.
Chanzo, dw.de/swahili  

0 comments: