Tuesday, 25 February 2014

MAREKANI KUPITIA UPYA UHUSIONO WAKE NA UGANDA

 Uganda_Gays_Leff_16b7f.jpg
Na Fadhy Mtanga
SERIKALI ya Marekani imeanza mchakato wa kuupitia upya uhusiano wake na Uganda, taifa la Afrika Mashariki baada ya rais wa nchi hiyo kutia saini mswada unaoharamisha vitendo vyote vya kishoga nchini humo.  Hapo jana, jijini Entebbe, rais wa Uganda aliweka saini katika msaada huo ili kuwa sheria rasmi ya Uganda.  Kitendo hicho kimelalamikiwa sana na mataifa ya Marekani na Uingereza kwa madai kinakiuka haki za kibinadamu.
 Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imetoa taarifa kupitia kwa waziri wake, John Kerry ikieleza kuwa serikali ya rais Barack Obama itahakikisha uhusiano wake na Uganda unazingatia sera yake ya kuzuia unyanyasaji wa aina yoyote.
 Katika taarifa hiyo iliyotumwa kwa barua-pepe kwenda kwenye gazeti la Daily Nation la Kenya, Kerry amesema, "Kwa kuwa sasa hii sheria imekwishapitishwa, tunaanza mchakato wa ndani kuhusiana na uhusiano wetu na Serikali ya Uganda ili kuhakikisha namna zote za mahusiano yetu, ikijumuisha misaada ya kimaendeleo zinaakisi dhima yetu ya kuondoa unyanyasaji na ubaguzi."
 Waziri huyo wa mashauri ya kigeni wa Marekani amepigia chapuo kufutwa kwa sheria hiyo.  "Hii ni siku ya msiba mkubwa kwa Uganda na wote wanaojali kuhusu haki za kibindamu.  Kimsingi, suluhisho pekee ni kufutwa kwa sheria hii."
 Kuwekwa sahihi kwa sheria hiyo kumewagutua Marekani, Uingereza na jumuiya zingine zinazopigia debe mashoga kupewa haki.  Tayari rais Barack Obama ametoa taarifa kupitia kwa katibu wake kuwa, "rais wa Uganda amefanya kitendo kichachostahili kujutiwa kwa kuwa ameirudisha nchi yake nyuma badala ya kusimamia uhuru na haki sawa kwa watu wake."
 Kerry, katika taarifa yake ameeleza wazi kuwa Marekani imekuwa ikiupinga mswada huo toka ulipofahamika miaka minne iliyopita.  Ameeleza zaidi kuwa sheria hiyo inakinzana na uwepo wa Tume ya Haki za Binadamu ambayo ipo kwa mujibu wa katiba ya Uganda.
 "Kutoka Nigeria hadi Russia na Uganda, tunafanya kazi ulimwengu mzima kuhamasisha na kulinda haki za kibidamu kwa watu wote.  Marekani itaendelea kusimama imara dhidi ya jitihada zozote kuwatenga, kuwaharamisha na kuwaadhibu wahanga wowote wake katika jamii yoyote ile."  Alisema Kerry.
 Kitendo hicho cha Museveni kimeibua hisia kali kutoka kwa baadhi ya taasisi za kimataifa ikiwemo makao makuu Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.  Tayari Katibu Mkuu Ban Ki-moon ameeleza azma yake ya kulijadili jambo hilo la kupinga ushoga pindi atakapokutana na balozi wa Uganda katika Umoja wa Mataifa.

0 comments: