>>TAARIFA YA KLABU ZOTE TANZANIA YATAKIWA TFF!
>>VPL: AZAM, ASHANTI UNITED KUCHEZA JUMATANO!
>>RAIS MALINZI KUZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI!
SOMA ZAIDI:
Release No. 032
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Februari 25, 2014
22 WAITWA TAIFA STARS KUIKABILI NAMIBIA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) limetangaza kikosi cha wachezaji 22 kwa ajili ya mechi ya kirafiki
ya kalenda ya FIFA dhidi ya Namibia (Brave Warriors) itakayochezwa
Machi 5 mwaka huu jijini Windhoek, Namibia.
Wachezaji walioitwa katika timu hiyo ni
makipa Deogratius Munishi (Yanga), Ivo Mapunda (Simba) na Mwadini Ally
(Azam). Mabeki wa pembeni ni Edward Charles (JKT Ruvu), Erasto Nyoni
(Azam), Hassan Mwasapili (Mbeya City) na Michael Aidan (Ruvu Shooting).
Mabeki wa kati ni Aggrey Morris (Azam)
na Kelvin Yondani (Yanga) wakati viungo ni Amri Kiemba (Simba), Athuman
Idd (Yanga), David Luhende (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Jonas Mkude
(Simba) na Mwinyi Kazimoto (Markhiya Sports Club, Qatar).
Washambuliaji ni Athanas Mdamu (Alliance
Mwanza), Haruna Chanongo (Simba), Khamis Mcha (Azam), Mbwana Samata (TP
Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Mrisho Ngasa (Yanga),
Ramadhan Singano (Simba) na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Congo- DRC).
Taifa Stars inayodhaminiwa na
Kilimanjaro Premium Lager itaingia kambini Machi 1 mwaka huu, kwenye
hoteli ya Accommondia inatarajiwa kuondoka Machi 3 mwaka huu kwenda
Windhoek.
Wachezaji ambao timu zao zinacheza mechi
za mashindano ya kimataifa na ligi wikiendi hii wataripoti kambini mara
baada ya mechi zao kumalizika.
TAARIFA YA KLABU ZOTE TANZANIA YATAKIWA TFF
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) zimewaagiza wanachama wake- vyama vya mpira wa miguu vya mikoa
kuwapatia orodha ya klabu zote za mpira wa miguu zilizosajiliwa katika
mikoa yao.
Orodha hiyo inatakiwa kujumuisha namba
ya usajili wa klabu, viongozi waliopo madarakani kwa sasa pamoja na
mawasiliano yao (namba za simu na anuani za email) na eneo yalipo makao
ya klabu husika.
Kwa utaratibu huo, vyama vya mikoa
vitakusanya taarifa za klabu zinazocheza ligi ya mikoa, lakini wakati
huo vinatakiwa kuwasiliana na wanachama wake (vyama vya wilaya) kupata
taarifa za klabu zinazocheza ligi za wilaya na baadaye kuziwasilisha
TFF.
Klabu ambazo taarifa zake zitakuwa
hazijawasilishwa TFF hadi Agosti mwaka huu hazitaruhusiwa kushiriki ligi
ya msimu wa 2014/2015 katika ngazi yoyote ile.
RAIS MALINZI KUZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), Jamal Malinzi atakuwa na mkutano na waandishi wa habari
juu ya programu ya mpira wa miguu kwa vijana.
Mkutano huo utafanyika kesho (Februari
26 mwaka huu) saa 5 asubuhi kwenye ofisi za TFF zilizopo ghorofa ya 3
katika Jengo la PPF Tower, mtaa wa Garden na Ohio.
AZAM, ASHANTI UNITED KUKIPIGA VPL
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania
ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho (Februari 26 mwaka huu) kwa
mechi moja itakayochezwa Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini
Dar es Salaam.
Mechi itazikutanisha timu za Azam
inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 37
dhidi ya Ashanti United iliyoko nafasi ya 12 kwa pointi zake 14.
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari na Mawasiliano
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 comments:
Post a Comment