Wednesday, 26 February 2014

BUNGE LA KATIBA: KILA MBUNGE ANA DAKIKA MOJA NA NUSU TU YA KUONGEA KATIKA SIKU 90!

 

Ndugu zangu,
Kwa Wabunge wetu wateule Bunge la Katiba kuendelea kupoteza muda kujadili posho na kanuni ambazo hazijakaa sawa mpaka sasa ni kuzidi kupoteza muda kwa kazi ambayo wananchi tulitarajia waende wakaifanye kule Dodoma; kujadili na kupitisha rasimu ya pili ya Katiba yenye kutokana na mawazo ya Wananchi.
Sijui kama kuna Wabunge wengi wateule wenye kujua, kuwa hata kama watakaa Dodoma kwa siku 90, bado, kwa hesabu za Kisayansi, hiyo ina maana ya dakika 54,000. Ukizigawa hizo kwa wajumbe 600 tu, unapata wastani wa dakika moja na nusu kwa siku ya kuongea kwa kila mjumbe. Ni kwa siku 90 na kwa kuchukulia kuwa watafanya kazi kwa saa kumi kwa siku, kuanzia Jumatatu mpaka Jumapili.
Hivyo, kwa hesabu hizo, nauona ukweli, kuwa hata hizo siku 90 hazitawatosha wajumbe wa Baraza la Katiba, endapo, sura ya hali itakavyokuwa Bungeni itakuwa kama inavyoonekana sasa. Hali ya mivutano na hasa kama Bunge hilo litaamua kufanya kazi ya kubadili vifungu vya rasimu hiyo na hata kuweka vipya.
Maana, kutahitajika mjadala mrefu. Na mjadala huo utatoka hata nje ya Bunge, kwa maana, wananchi nao watakuwa wakijadili kupitia vyombo vya habari na kuathiri upepo wa majadiliano ndani ya Bunge. Hivyo basi, kutakuwa na hali ya kuahirishwa vikao mara kwa mara na siku pia kuongezeka.
Nahofia pia, kuwa Wabunge wazoefu kwenye kuzungumza ndio watakaozungumza, na hivyo basi, watakuwa wamekula muda wa wenzao. Na matokeo yake, ni ukweli kuwa, kuna wabunge walioko Dodoma sasa, watakaozimaliza siku 90 kwa kuishia kupiga kura tu, na si kujadili Katiba wakasikika na kuonekana na waliowatuma kwenda Dodoma.
Naam, tutayaepusha haya, ambayo kimsingi ni aibu kwa taifa, kama tutatanguliza hekima na busara na zaidi kwa kutanguliza maslahi ya umma, na si ya binafsi, makundi au vyama vya siasa. 
Imeandikwa na mwandishi maarufu nchini Tanzania
Maggid Mjengwa,
Iringa.
0754 678 252 (

0 comments: