Najua matatizo
yanayoikabili kata hii; ni maji, umeme, barabara na mawasiliano, nipe
kura nimalizie pale alipoishia Dk William Mgimwa
KATIBU
wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilayani Mufindi, Miraji Mtaturu amewataka wananchi
wa Jimbo la Kalenga kujua kiasi cha fedha anazolipwa Dk Wilbroad Slaa kila
mwezi ili waoanishe na harakati zake anazodai zinalenga kupinga ufisadi.
Dk
Slaa ni Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema); yupo
wilayani Iringa akiongoza kampeni za kumnadi Grace Tendega anayegombea ubunge
katika jimbo hilo kupitia chama hicho.
Katika
mikutano ya kumnadi mgombea wao Godfrey Mgimwa iliyofanyika katika vijiji vinne
vya kata ya Kiwele jana, Mtaturu alisema Dk Slaa ndiye kiongozi wa chama cha
siasa nchini anayelipwa fedha nyingi kuliko mwingine yoyote.
Alisema
katika mazingira ambayo wanachama na baadhi ya viongozi watendaji wa Chadema wanatumia
fedha zao za mifukoni kujenga chama hicho, Dk Slaa analipwa zaidi ya Sh Milioni
10.
“Muulizeni
akija hapa ni kiasi gani analipwa kila mwezi; aliwekwa sharti la kulipwa
kiwango kinachofanana na kile wanacholipwa wabunge kama sharti la kukubali
kugombea urais badala ya ubunge katika Uchaguzi Mkuu uliopita,” alisema.
Alisema
mtu anaweka masharti na kutanguliza maslai yake mbele katika kazi ya
kuwatumikia wananchi hafai kuwa kiongozi na ni muhimu kuwa makini na kauli
zake.
Katika
mikutano iliyofanyika katika vijiji vya Mgera, Kiwele, Mfyome na Kitapilimwa,
Mtaturu aliwaomba wananchi wa jimbo la Kalenga kutofanya makosa katika uchaguzi
huo.
“Kazi
anayokwenda kumalizia Godfrey Mgimwa ilikwishaanza kufanywa na marehemu Dk
William Mgimwa; mpeni kura zenu zote ili akamalizie utekelezaji wa Ilani ya
CCM,” alisema.
Akijinadi
kwa wapiga kura wa kata hiyo, Mgimwa alisema “sijagombea nafasi hii ili
niharibu kazi inayoendelea kufanywa na chama changu, sikugombea ili kupotosha
ukweli wa yale yote yanayoendelea kufanywa, ninagombea kwasababu nataka
kumalizia kazi,” alisema.
Alisema
akiwa mbunge katika jimbo hilo atahakikisha kwa kushirikiana na wapiga kura
wake anamalizia utekelezaji wa ahadi mbalimbali za maendeleo zilizotolewa na
CCM kupitia Ilani yake ya 2010 na zile zilizoachwa na marehemu baba yake.
“Najua
katika kata hii kuna changamoto zinazoendelea kupatiwa ufumbuzi; nipeni nafasi
nikazishughulikie,” alisema na kuzitaja changamoto hizo zikihusisha sekta ya
maji, afya, barabara, pembejeo, elimu na mawasiliano.
Mwenyekiti
wa CCM Wilaya ya Iringa, Delfina Mtavilalo alisema katika uchaguzi huo Chadema
itashika nafasi ya pili kama inavyojidhihirisha kupitia salamu yao.
“Vidole
viwili havina maana nyingine zaidi ya namba mbili na ndio maana kila wanapopita
wanaonesha wao ni namba mbili kwa kuonesha ishara ya vidole hivyo,” alisema.
Katibu
wa CCM Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga alisema wananchi wa Kalenga watakosea kama
watampa ubunge mtu ambaye hawajui watampata wapi.
Alisema
CCM inawajibika kwa wananchi na ndio maana ina mfumo wa uongozi kutoka ngazi ya
tawi hadi taifa tofauti na Chadema.
Akiahidi
kutoa zawadi ya fedha kwa wananchi wa kata ya Kiwele kama watamtajia safu ya
viongozi wa chama hicho katika jimbo hilo, Mtenga alisema bado hakiaminiki na
ndio maana kinakosa viongozi katika nafasi zake mbalimbali.
“Ulizeni
kama kina viongozi wa kuchaguliwa kwenye kata zake na kama kina uongozi wa
wilaya uliokamilika,” alisema.
|
0 comments:
Post a Comment