Wednesday, 26 February 2014

MADINI YA TANZANITE YANGA’RA BANGKOK NCHINI CHINA

1Baadhi ya madini ya Tanzanite ambayo yanapatikana katika mabanda mbalimbali katika maonesho ya 53 ya Kimataifa ya Bangkok Gems and Jewelry Fair. 2Mfanyabiashara  wa madini na Afisa Masoko wa Kampuni ya Tom Gems Tanzania, akimwonesha mgeni aliyefika katika banda la Tanzania kuona madini ghafi ya Tanzanite  yanayozalishwa Tanzania pekee. Wageni wengi wamefika katika banda hilo kuona Tanzanite halisi kutoka Tanzania. 3 (2)Mwenyekiti wa Madini ya Viwandani Bw. Kassim Iddi Pazi, akimwonesha mgeni madini ya Ruby. Kutokana na maelezo ya Bw. Pazi, ameeleza kuwa, madini hayo yametoka katika maeneo ya Winza Dodoma na Matombo Morogoro. 4Mfanyabiashara wa Madini kutoka Kampuni ya Tom Gems Bw.Benjamin Mtalemwa akimwonesha mgeni madini mbalimbali alipotembelea banda la Tanzania. Wanaoshuhudia kutoka kulia ni Mthamini wa Madini kutoka Wizara ya Nishati na Madini Bw. Edward Rweymamu, Wa pili kulia ni Afisa Madini kutoka Shirika la Madini Tanzania (STAMICO). Bw. Peter Maha, na  wa kwanza kulia  ni Afisa toka Wizarani Bibi. Margareth Muhony.
 …………………………………………………………………
Na Asteria Muhozya, Bangkok
Madini ya Tanzanite yamekuwa kivutio kikubwa katika maonesho ya 53 ya Kimataifa ya‘’Bangkok Gems and Jewelry Fair’’, yanayoendelea katika eneo la kibiashara la ‘Impact Challenger’, jijini Bangkok. 
Madini ya Tanzanite yanayozalishwa nchini Tanzania pekee duniani, yamekuwa kivutio  kikubwa kwa wageni wanaotembelea maonesho hayo ikiwemo  wauzaji, wanunuzi na wafanyabiashara ambao wamefika  katika banda la Tanzania kutaka kuona Tanzanite halisi kutoka Tanzania. 
Aidha, pamoja na kwamba madini ya Tanzanite yanazalishwa na  Tanzania pekee, lakini katika maonesho hayo ya Bangkok, madini hayo yanapatikana kwa kiasi kikubwa katika mabanda  ya washiriki kutoka nchi mbalimbali  duniani jambo ambalo linaonesha namna madini hayo yalivyo na muhimu katika sekta zakibiashara na kiuchumi.
Akizungumzia suala la uwepo  wa madini ya Tanzanite kwa kiasi kikubwa katika soko la kimataifa, na katika maonesho hayo, Kamishna Msaidizi wa Madini , Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Hamis Komba, ameeleza kuwa,  uwepo wa Tanzanite katika soko la kimataifa unaashiria mahitaji makubwa ya madini hayo duniani na umuhimu wake katika kuchangia  ukuaji wa uchumi wa Tanzania, na nchi nyinginezo ikiwemo thamani yake katika soko la kimataifa na upekee wake.
Aidha, , aliongeza kuwa, hiyo ni changamoto katika uthibiti wa madini hayo katika soko la kimataifa kutokana  na uwiano wa takwimu  za kiasi cha madini kinachotoka kwa kufuata taratibu za usafirishaji madini hayo nje ya nchi na uwingi halisi unaoonekana  katika soko la Kimataifa. 
“Uwiano wa takwimu za uzalishaji Tanzania na idadi halisi ya madini iliyopo katika maonesho ya  kimataifa ni tofauti. Hii ni changamoto katika udhibiti wa madini haya” Amesema Kamishna Komba.
Hivyo, ameongeza kuwa, Serikali inalifanyia kazi suala hili kwa lengo la kufanikisha usimamizi na biashara endelevu ya madini ya Vito na usonara.
Mbali na madini ya Tanzanite  kuwa kivutio, katika banda la Tanzania, vinyago vinavyotengenezwa kutokana  na mawe aina  ya  Zoisite, Basalt, Limestone, Travertine, Granite na White marbale yanayopatikana Tanzania  ambayo  yametengenezwa mapambo mbalimbali ya majumbani yamekuwa kivutio kikubwa katika maonesho hayo kwa wageni waliotembelea banda la Tanzania kutoka nchi za Ulaya na Asia, akiwemo pia Rais  wa Shirikisho la wafanyabiashara wa vito na usonara Bw. Somchai Phornchindarak, ambaye pia alitembelea Banda la Tanzania na kuonesha kuvutiwa na kushangazwa na mapambo hayo.

0 comments: