Waasi wa kundi la kikristo la Anti Balaka katika Jamhuri ya Afrika ya Kati wametishia kuwaua mamia ya waislamu wanaojificha katika kanisa moja kama hawataondoka nchini humo katika kipindi cha wiki moja ijayo.
Wanajeshi wa kulinda amani wapatao 30 kutoka Cameroon walilazimika hapo jana kufyatua risasi hewani ili kuwatawanya wapiganaji wa Anti Balaka waliokuwa wamekusanyika nje ya kanisa hilo la Kikatoliki wakipania kuwaua waislamu hao ambao wamekimbilia katika kanisa hilo kuokoa roho zao.
Milio hiyo ya risasi iliwaogofya watoto waliokimbia kujinusuru na vilio vya watu hao waliojawa na uoga vilisikika vikirindima katika kanisa hilo.Wanajeshi hao wa kulinda amani kwa sasa ndiyo tegemeo la pekee kwa waislamu hao wapatao 800 dhidi ya kushambuliwa na magenge yanayotaka kuwaua.
Wapiganaji wa Anti Balaka tayari
walionekana wakiwa na mitungi ya lita 40 ya petroli ambayo wametishia
kutumia kulichoma kanisa hilo.Kasisi wa kanisa hilo Justin Nary ambaye
anatoa hifadhi kwa waislamu hao anajua analengwa na waasi hao.
Waasi walizingira kanisa kuwasaka waislamu
Kasisi Nary amesema wapiganaji hao wa
Anti Balaka wamemtishia maisha mara nne kwa kumulekezea mtutu wa bunduki
na wamempigia simu kumuonya kuwa punde tu wanajeshi wa kulinda amani
wataondoka,watamuua.
Baadhi ya wanaotafuta hifadhi katika
kijiji hicho cha Guen wametoroka baada ya kiasi ya waislamu 70 kuuawa
katika siku za hivi karibuni.Waislamu na wakristo walikuwa wakiishi kwa
amani tangu jadi hadi kundi la waasi la kiislamu kutoka Kaskazini mwa
nchi hiyo lilipoipindua serikali na kulitumbukiza taifa hilo katika
ghasia.
Kundi hilo la kiislamu la Seleka
linashutumiwa kwa mauaji katika vijiji vya wakristo katika taifa
hilo.Viongozi waliosaidiwa na Seleka kuingia madarakani walipoondolewa
madarakani mwezi Januari,ilichochea mashambulizi ya kulipiza kisasi
kutoka kwa kundi lililoibuka la Anti Balaka.
Mauaji yaripotiwa katika miji mingine
Mji mkuuu Bangui ambao ulikuwa ni
kitovu cha maasi na ghasia tangu mwezi Desemba kwa sasa hali inaonekana
kudhibitiwa kwa kiasi fulani lakini mauaji yanayofanywa kwa misingi ya
kidini yanaendelea kuripotiwa katika miji mingine nchini humo.
Majeshi ya Ufaransa na ya umoja wa
Afrika yaliyoko nchini humo kudhibiti hali hayatoshi kukidhia mahitaji
ya kiusalama na kiulinzi yanayohitajika kwa dharura.
Umoja wa Mataifa umeiomba Jumuiya ya
kimataifa kuchukua hatua kabambe na za dharura kuisaidia Jamhuri ya
Afrika ya Kati kujikwamua kutoka kwa mzozo mbaya unaotishia
kulisambaratisha taifa hilo.
Bunge la Ufaransa hii leo linatarajiwa
kupiga kura kuidhinisha kuendelea kusalia kwa jeshi lake nchini humo
hadi mwezi Februari mwaka ujao wakati ambapo Jamhuri ya Afrika ya Kati
itafanya chaguzi.
Waziri wa ulinzi wa Ufaransa Jean Yves
Le Drian amekiri kuwa itachukua muda mrefu kuliko walivyotarajia
kurejesha udhabiti nchini humo kutokana na kiwango cha juu cha uhasama
na ghasia.Maelfu ya watu wameuawa tangu Desemba na zaidi ya watu milioni
moja wameachwa bila makaazi.
Chanzo, dw.de.com/swahili.
0 comments:
Post a Comment