Na Fadhy Mtanga
IKIWA ni
siku chache tu tokea rais wa Uganda, Yoweri Museveni kutia saini sheria
inayoharamisha ushoga nchini Uganda, serikali ya Japan imesema
haitositisha misaada yake kwa nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Kauli
hiyo imetolewa jana na balozi wa Japan nchini Uganda, Junzo Fujita.
Fujita aliyasema hayo baada ya kuweka saini makubaliano
yatakayoziwezesha jamii za mashariki na kaskazini ya Uganda kunufaika na
msaada unaofikia kiasi cha dola za Kimarekani 203,183 kupitia mpango wa
Grant Assistance for Grassroots Projects.
"Jambo
hili (sheria dhidi ya ushoga) na misaada ni vitu tofauti. Kwa mtazamo
wangu, watu wanaathirika na wanahitaji maji safi. Hatuwezi kufumba macho
yetu eti kwa sababu ya jambo hilo (sheria dhidi ya ushoga)." Alisema
Fujita.
Hata
hivyo, balozi huyo alikiri wazi kuwa namna Japan inavyolichukulia suala
la ushoga inatofautiana kidogo na nchi zingine wahisani kama Marekani na
Uingereza. Akakubali kuwa kutiwa saini kwa sheria hiyo nchini Uganda
kumechochea hasira kwa jumuiya ya nchi wahisani.
Lakini,
Fujita akaweka wazi msimamo wa Japan akisema, "Tunawasiliana na serikali
yetu nyumbani kuhusiana na hili – ili tufahamu kama tunapaswa kuungana
na nchi wahisani zingine ama la."
Akasema
kuwa nchi zote ikiwemo Uganda, zinawajibika kutii matakwa ya mikataba ya
kimataifa ya haki za kibinadamu ambayo imeiridhia.
Wahisani wakasirishwa
Nchi
wahisani zimeonesha kukasirishwa na hatua hiyo ya serikali ya Uganda.
Kwa mujibu wa sheria mpya dhidi ya ushoga iliyotiwa saini na Yoweri
Museveni siku ya Jumatatu jijini Entebbe, kosa la mapenzi ya jinsia moja
litamfanya mtuhumiwa anayepatikana na hatia hiyo kuhukumiwa kifungo cha
maisha jela.
Waziri wa
Fedha wa Sweden, Anders Borg ameionya Uganda kuwa hatua hiyo itaiathiri
Uganda kiuchumi. Aliyasema hayo Jumanne wiki hii akiwa nchini Uganda
kama sehemu ya ziara yake kwa nchi za Afrika Mashariki kwa madhumuni ya
kupitia ukuaji wa uchumi katika eneo hilo.
"Sasa
tunapitia upya mipango yetu ya usaidizi kwa Uganda na ni wazi
tutalizingatia hili." Alisema Borg. Akaongeza kuwa tayari
amekwishaifikisha hoja yake kwa Waziri wa Fedha wa Uganda, Maria
Kiwanuka na Waziri Mkuu, Amama Mbabazi. Mkutano wake wa mawaziri hao
waandamizi wa serikali ya Uganda ulifuatia mkutano wake na wanaharakati
wa ushoga nchini humo.
Wakati
hayo yakijiri, tayari Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Marekani, John
Kerry ametoa taarifa maalumu kuwa serikali yake inapitia upya uhusiano
wake na Uganda ili kuondoa misaada yake kufuatia kusainiwa kwa sheria
hiyo ambayo Marekani inasema ni ya kinyanyasaji yenye kukandamiza haki
za kibinadamu.
Vile
vile, nchi za Norway, Denmark na Uholanzi zimesimamisha rasmi misaada
yake kwenye bajeti ya Uganda siku hiyo hiyo ya Jumatatu mara tu Yoweri
Museveni alipotia saini sheria hiyo.
Uingereza
nayo imeonesha nia ya kuacha kuisaidia Uganda huku Umoja wa Mataifa nao
ukieleza wazi kuudhiwa na sheria hiyo. Katibu Mkuu Ban Ki-moon anapigia
chapuo kufutwa haraka kwa sheria hiyo.
0 comments:
Post a Comment