Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Liberatus Sabas.
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Watu
wanne ambao bado hawajafahamika wanaume wanaokadiriwa kuwa na umri kati
ya miaka 25 hadi 35 wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wameuawa baada ya
kupigwa risasi na askari Polisi. Tukio hilo lilitokea jana tarehe
21.02.2014 muda wa saa 1:00 jioni katika bar moja iitwayo Pama iliyopo
maeneo ya Makao Mapya jijini hapa.
Akithibitisha
kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna
Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Liberatus Sabas alisema kwamba,
tukio hilo lilitokea mara baada ya jeshi la polisi Mkoani hapa kupata
taarifa toka kwa raia wema kwamba watu hao walikuwa wanapanga kwenda
kufanya tukio la uhalifu katika kituo kimojawapo cha kuuzia mafuta
kilichopo jijini hapa ambapo ufuatiliaji wa taarifa hiyo ulianza.
Ilipofika
muda huo askari hao walikwenda katika bar hiyo na mara baada ya
majambazi hao kuwaona askari hao walihisi wanafuatiliwa ndipo mmojawao
ghafla alitoa bastola na kufyatua risasi tatu ambapo moja ilimparaza
askari mmoja aitwaye F. 1416 D/Ssgt Richard katika mkono wake wa kushoto
“Kufuatia
hali hiyo askari nao waliamua kujibu mapigo kwa kupiga risasi ambapo
wanne kati ya watano walijeruhiwa na mmojawao alifanikiwa kukimbia akiwa
na silaha inayosadikiwa kuwa ni SMG”. Alisema Kamanda Sabas.
Kamanda
Sabas alisema kwamba, majambazi hao walifariki dunia wakiwa njiani
kuelekea hospitali ya Mount Meru kwa ajili ya matibabu na miili yao
imehifadhiwa hospitalini hapo kwa ajili ya utambuzi toka kwa ndugu na
jamaa wa karibu.
Aidha
Kamanda Sabas alisema, katika eneo la tukio askari hao walipata bastola
moja aina ya Star yenye namba 42640 FNH PISTOLE MODEL KAL 7.65 ikiwa na
risasi tatu katika magazine, maganda matatu ya risasi pamoja na begi
moja dogo la mgongoni lenye rangi nyekundu likiwa na risasi nne hivyo
kufanya jumla ya risasi saba kupatikana.
Bado
Jeshi la Polisi Mkoani hapa linaendelea na upelelezi kuhusiana na tukio
hilo ikiwa ni pamoja na kumtafuta mtuhumiwa mmoja aliyekimbia.
Kufuatia
tukio hilo Kamanda Sabas aliendelea kuwashukuru wananchi wa Arusha kwa
ushirikiano wao mkubwa wanaoutoa kwa jeshi la Polisi Mkoani hapa na
kuwasihi waendelee kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu hali
itakayosaidia kukomesha matukio ya uhalifu mkoani hapa.
0 comments:
Post a Comment