Serikali inapenda kuwaarifu waombaji wa
nafasi za kazi kwa tangazo la tarehe 27 Novemba, 2013 wa kada za
Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Udereva kuwa usaili utaanza tarehe 4 Machi,
2014 takriban katika mikoa yote Tanzania Bara na Zanzibar.
Katibu
wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Bw. Xavier Daudi
amesema hayo leo ofisini kwake wakati akiongea na baadhi ya wadau
waliomtembelea kwa lengo la kufahamu masuala mbalimbali ya uendeshaji wa
mchakato wa ajira serikalini.
Amesema
usaili huo unaoanza tarehe 4 Machi katika mikoa takribani yote nchini
utahusisha jumla ya wasailiwa 6,087 wa fani za Kilimo, Mifugo, Uvuvi na
udereva kwa kada ambazo sio za Maofisa. Amefafanua kuwa vigezo vya
kupanga mikoa ya usaili vimetokana na anwani ambazo waombaji
waliwasilisha katika barua zao za maombi husika ya kazi.
Daudi
alibainisha kuwa kila mwombaji aliyekidhi vigezo na kuchaguliwa kwa
ajili ya usaili anapaswa kwenda kufanyia usaili katika mkoa aliopangiwa
kama anwani yake inavyoonyesha katika tangazo kwenye tovuti ya
Sekretarieti ya Ajira, isipokuwa kwa waombaji wa mkoa wa Katavi wao
wataenda kufanyia usaili mkoa wa Rukwa na waombaji waliotumia anwani za
mkoa wa Singida wao watafanyia usaili mkoa wa Manyara kutokana na sababu
zisizozuilika.
Aliongeza
kuwa kwa mwombaji ambae hatazingatia anwani, siku na muda aliopangiwa
na kuamua kwenda mkoa mwingine tofauti na utaratibu uliopangwa ajue wazi
hatasailiwa kwa kuwa ratiba na idadi ya majopo ilishapangwa kwa kila
mkoa na haitabadilishwa ili kuweza kurahisisha kazi hiyo kukamilika kwa
ufanisi.
Aidha, amewataka waombaji wote wa tangazo hilo kutembelea tovuti ya Sekretarieti ya Ajira ambayo ni http://www.ajira.go.tz/
wao wenyewe ili kuweza kujua kiundani endapo wamechaguliwa kufanya
usaili, kufahamu tarehe, mahali na muda wa kuanza usaili ili kuepuka
usumbufu usiokuwa na lazima.
Daudi
aliendelea kufafanua kuwa kwa waombaji waliotumia anuani za mkoa wa Dar
es Salaam kwa nafasi ambazo sio za maofisa usaili utafanyika tarehe 11
Machi, 2014. Aidha, kwa nafasi za Maofisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wote
usaili wao utafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 10 hadi 14
Machi, 2014.
Katibu
amewataka waombaji wote kuhakikisha pindi wanapoenda kwenye usaili
wawe wamejiandaa vya kutosha ikiwemo kubeba nyaraka muhimu hususani
vyeti halisi vya taaluma zao maana vitahitajika kwa ajili ya uhakiki
siku ya usaili. Aidha, amewasihi waombaji wa matangazo mengine ya nafasi
za kazi kuwa na subira wakati uchambuzi ukiendelea na pindi
utakapokamilika wahusika watataarifiwa.
Alimaliza
kwa kuwasisitiza wadau wa Sekretarieti ya Ajira kuwa pindi wanapoona
matangazo ya kazi, ikiwemo kuitwa kwenye usaili au kupangiwa vituo vya
kazi katika vyombo mbalimbali vya habari hususani baadhi ya mitandao ya
kijamii wajiridhishe kwanza kwa kuangalia taarifa hizo katika tovuti ya
Sekretarieti ya Ajira, ili kuepuka taarifa zisizokuwa za kweli ambazo
zimekuwa zikitolewa nyakati nyingine na baadhi ya watu wasio waaminifu
kwa lengo la kupotosha Umma.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini.
Ofisi ya Rais-Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma. 21 Machi, 2014
Kwa maelezo zaidi; wasiliana na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
0 comments:
Post a Comment