Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Dodoma. Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amesema atagombea uenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba kwa sababu anaamini kuwa ana sifa za kutosha.
Hii ni mara ya kwanza kwa Sitta ambaye alikuwa Spika wa Bunge la Tisa kuweka wazi uamuzi wake huo. Mwingine anayetajwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa zamani na Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge
.
Sifa za mtu anayepaswa kuongoza Bunge
hilo ni kuwa na shahada ya sheria kutoka katika chuo kinachotambulika
pia kuwa na uzoefu wa kuendesha mijadala kama ya Bunge.
Akizungumza na gazeti hili jana, Sitta
alisema pamoja na propaganda chafu zinazoenezwa dhidi yake, hatakata
tamaa na kwamba ataendelea na msimamo wake huo ili nchi ipate Katiba
bora.
"Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
imeainisha sifa za mtu anayetakiwa kuwa mwenyekiti na mimi nina sifa na
nina mipango mizuri ya kuwafanya Watanzania wapate Katiba bora kama
ndoto ya Rais wetu (Jakaya Kikwete) ilivyo," alisema.
Alipoulizwa kuhusu njama za kumzuia
asigombee nafasi hiyo, Sitta alisema "Haishangazi watu hao kutumia mbinu
chafu... Hawana maadili, ndiyo maana wananihofia lakini sishtuki hata
kidogo."
Sitta ambaye pia ni mbunge wa Urambo
Mashariki (CCM), alisema wabaya wake wamekuwa wakieneza maneno ya uongo
kwamba ikiwa atakalia kiti hicho, atasimamia mpango wa Serikali tatu.
"Wanasema Sitta ataruhusu Serikali
tatu, sasa nashangaa maana wajumbe ndiyo wenye mamlaka hayo... wanaeneza
propaganda kuwa nina mkataba na wapinzani ndiyo maana wananiunga mkono.
Wanasema mambo ya ovyo kabisa," alisema.
Sitta alisema wapinzani kama walivyo
wajumbe wengine kutoka CCM na makundi mengine, wanamuunga mkono kwa kuwa
wanaamini akikalia kiti hicho ataendesha Bunge hilo kwa misingi ya
uwazi na haki.
"Mimi sina mkataba na wapinzani ila
wao kama watu wengine wananiunga mkono kwa sababu wanajua nitatenda
haki, nina rekodi nzuri katika kuliendesha Bunge la Tisa wala hiyo haina
mashaka," alisisitiza Sitta.
Sitta na Chenge
Kumekuwa na msuguano na kampeni za
chini chini kati ya kundi la Sitta na Chenge, lakini habari
zilizopatikana jana kabla ya Sitta kutangaza kuwania nafasi hiyo,
zilisema CCM walikuwa wakikusudia kuwaondoa makada hao, na kumpendekeza
Mathias Chikawe badala yao
Ilielezwa kuwa hatua hiyo imefikiwa
kutokana na mpasuko mkubwa ndani ya chama hicho unaotokana na wapambe wa
makada hao kuanza kupakana matope.
Hata hivyo Chikawe alisema hana
taarifa yoyote kuhusu mpango huo. "Ahaaa! Sina taarifa hiyo, sijawahi
kufikiria kushika nafasi hiyo, wewe (mwandishi) ndiyo unaniambia na
nimeshtuka sana, lakini nitafuatilia," alisema Chikawe.
Kwa upande wake, Chenge juzi alisema
hana sababu ya kulumbana na watu aliowaita kuwa hawataki kuelewa na
kwamba tayari CCM kilikuwa kimetoa mwelekeo wake.
Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na
Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema chama hicho hakijatoa msimamo wa mtu
kinayetaka agombee nafasi hiyo kwani hakuna kikao chochote
kilichojadili suala hilo.
"Kama uamuzi unafanywa, lazima vikao
vya chama vikae, lakini hadi sasa kwa uelewa wangu hakuna kikao chochote
cha chama ambacho kimeketi na kuamua suala hilo," alisema Nnauye.
Kauli ya Nnauye iliungwa mkono na ile
ya Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, William Lukuvi ambaye alisema chama
hakijatoa mwongozo wowote kuhusu suala hilo kwa kuwa muda wake bado.
"Chama hakijatoa mwongozo wowote ingawa tunajua watu wameanza kuumana kwa hilo, wako kama saba," alisema Lukuvi.
Lukuvi ambaye pia ni Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), alikuwa akijibu tuhuma
zilizotolewa dhidi yake kwamba ndiye anayeshawishi Sitta asiwe mmoja wa
wagombea katika kinyang'anyiro hicho ili kulinda mwonekano wa Spika wa
Bunge, Anna Makinda.
"Wanahofia endapo Sitta atafanikiwa
kupata uenyekiti na kuendesha vizuri Bunge na Makinda akaja kuendesha
Bunge la Bajeti ataonekana kupwaya sana," kilisema chanzo chetu.
Lukuvi alikanusha kuhusika na mpango
huo akisema: "Mimi nahusika vipi kwenye hilo. Kwanza kama chama
hatujatoa mwongozo lakini hatuwezi kutoa mwongozo kabla Bunge halijatoa
kanuni za namna ya kumpata mwenyekiti."
Lukuvi alikiri kufahamu kuwapo kwa
vita ya uenyekiti, lakini akasema yeye haoni mantiki ya kuhusishwa
kwake. "Mimi najua watu wameshaanza kuumana lakini kwa nini sasa, wakati
hata kanuni hazijatoka na chama hakijatoa mwongozo," alihoji
0 comments:
Post a Comment