Thursday, 9 January 2014

WAKULIMA ,MWAKALA WAMAHINDI WAMPA WAKATI MGUMU WAZIRI WA KILIMO,CHAKULANA USHIRIKA ADAM MALIMA

 
Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima

Serikali imesema itatoa uamuzi wa kuwalipa ama kuwarudishia mahindi mawakala na wakulima wa mikoa ya Singida na Dodoma baada ya wiki mbili.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, mawakala na wakulima wa mahindi katika mikoa hiyo waliandamana wakiwa na malori ya mizigo hadi Ofisi za Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula Kanda ya Kati (NFRA) kwa ajili ya kuishinikiza serikali kuwalipa deni lao la Sh. bilioni 2. 6.


Mawakala hao waliandamana kwa lengo moja la kutaka serikali iwalipe fedha zao au waruhisiwe kuchukua tani zao 4,000 za mahindi ili wakaziuze kwa watu wengine.

Kauli hiyo ilitolewa juzi mjini hapa na Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima ambaye aliwasili kwa ajili ya kusikiliza malalamiko ya mawakala na wakulima hao.

Malima alisema serikali itatoa kauli ya kuwalipa mawakala hao baada ya wiki mbili na iwapo itashindikana kuwalipa itaandikishiana nao mkataba wa kuwarudishia mahindi yao.


“Mimi naendelea kuwasiliana na Hazina, Waziri Mkuu na Wizara ya Fedha...baada ya wiki mbili nitakuwa na jibu la kulipwa fedha zenu au kurudishiwa mahindi,” alisema.

Alisema hadi sasa serikali inadaiwa Sh. bilioni 9.3 na mawakala wa mahindi kutoka mikoa mbalimbali nchini.

Aidha, Malima ambaye aliongozana na jopo la maofisa kutoka wizarani alikiri kuwa serikali kupitia Hazina kwa sasa haina fedha ya kulipa fedha hizo kwa mawakala mbalimbali wa mahindi nchini.


“Kumbukeni kuwa siyo nyie tu ambao mnatudai tunadaiwa na Katavi, Arusha, Rukwa na mikoa mingine pia...na mpaka sasa Wizara ya Fedha haijatuhakikishia ni kiasi gani itatoa kwa ajili ya kuwalipa,” alisema

Kutokana na hali hiyo, Malima aliiagiza NFRA kuweka rasilimali zake rehani katika Taasisi fedha ili waweze kupata mkopo wa kulipa deni hilo.

Baada ya Malima kutoa jibu hilo, mawakala na wakulima hao walionyesha kutoridhishwa na majibu ya Naibu Waziri na kutaka kurudishiwa mahindi yao.


Akizungumza Ally Ramadhani ambaye ni wakala wa mahindi, alisema iwapo zimenunuliwa tani za mahindi 22,000 na serikali ilikuwa na uwezo wa kununua tani 15,000 na uwezo wa kuwalipa mawakala fedha zao haina kwa nini isirudishe mahindi.


Kufuatia malumbano hayo yaliyochukua muda wa saa mbili, ilimlazimu Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi kutumia hekima kwa kuitaka wizara hiyo kutumia muda wa siku 14 ili kuwalipa mawakala na wakulima hao haki yao. 
SOURCE: NIPASHE
10th January 2014

Related Posts:

0 comments: